Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Trafiki Kinondoni kuanza ukaguzi wa vyeti kwa madereva

11372 Ukaguzi+pic TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika jitihada za kukabiliana na ajali za barabarani Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Kinondoni (RTO) Sadick Msangi amesema wataanza kufanya ukaguzi wa vyeti kwa madereva wote wa vyombo vya moto kuanzia Jumatatu.

Hayo ameyasema leo Julai 13, 2018 wakati wa zoezi la utoaji elimu kuhusu alama barabarani kwa madereva wa daladala na bodaboda katika stendi ya Makumbusho jijini hapa.

Amesema ukaguzi huo unalenga kuwabaini madereva waliogushi leseni na wasiojua sheria za barabarani.

"Hatutaki kuona leseni yako tu bali tunataka kujiridhisha kama kweli umesoma chuo cha udereva cheti unacho na unajua sheria za barabarani na hatuwezi kusema muda ni mdogo kwa sababu mpaka unaendesha gari unaamini kuwa una vigezo," amesema Msangi.

Amesema kuwepo kwa madereva wasio na weledi kimekuwa ni chanzo cha ajali za barabarani za kila mara jambo ambalo linapoteza nguvu kazi ya taifa na kusababisha ulemavu kwa watu.

"Na msako huu utafanyika kwa miezi minne ili kuwaondoa wale wote wenye tabia za ajabu barabarani, wanaosababisha ajali kwa kujua au kutojua," amesema Msangi.

Amesema wale watakaobainika hawana vyeti watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva Tanzania (TADWU), Shaban Mdemu aliliomba jeshi la polisi kuwachukulia hatua askari wote walio na tabia ya kuwatafutia leseni madereva wasio na vigezo.

"Kama anataka leseni akasome siyo afanue ujanja ujanja jambo ambalo linahatarisha maisha ya watu na usalama wa mali," amesema Mdemu

Chanzo: mwananchi.co.tz