Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tozo za paka, bata mjadala

33771 Pic+bata Tanzania Web Photo

Fri, 28 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Halmashauri ya Jiji la Tanga imetolea ufafanuzi wa tangazo lake linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na mapendekezo ya tozo mbalimbali ikiwamo kwa wanaofuga mifugo aina ya paka, kuku na bata, ikisema si mpya bali zilikuwapo kwa miaka mingi ya nyuma.

Tozo zinazoonekana katika tangazo linalosambaa mitandaoni lililosainiwa na kugongwa muhuri na mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Msambweni, ni kodi ya majengo Sh20,000 hadi Sh200,000, tozo za takataka Sh5,000 kwa kaya kwa mwezi, wauza maduka na baa Sh20,000 kwa mwaka na waendesha bodaboda Sh 10,000.

Nyingine ni baiskeli na mikokoteni Sh10,000, wauza chipsi Sh10,000, waanika machicha, wauza samaki na mihogo Sh10,000, wafugaji ng’ombe, mbuzi Sh 20,000 kwa mwaka, wafugaji paka, kuku, bata Sh10,000 kwa mwaka, mama lishe Sh10,000 kwa mwaka na vibali vya sherehe Sh25,000 kila tukio.

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mhina Mustapher (Selebos) ameiambia Mwananchi kwamba, mapendekezo ya tozo hizo yamepelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kuzijadili na kupendekeza zenye kufaa na zisizofaa ili zipelekwe kwenye baraza la madiwani kwa ajili ya kutoa baraka kabla ya kutumika kwa zitakazokubaliwa.

Aliwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kuhusiana na tozo hizo kwa kuwa ni utaratibu wa kawaida ndiyo maana wamepelekewa wazijadili na zitakazoonekana hazifai zitaondolewa ili halmashauri iweze kuboresha mapato yake ya ndani.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Daud Mayeji alisema kitendo cha mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Msambweni kusaini waraka huo, kuugonga mhuri na kisha kuusambaza mitandaoni ni kinyume cha sheria na taratibu za kiutendaji.



Chanzo: mwananchi.co.tz