Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tishio jipya Dodoma, wimbi wanafunzi kuacha shule

Wanafunzi Kuachaaaaa.png Tishio jipya Dodoma, wimbi wanafunzi kuacha shule

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati ripoti ya BEST inayotolewa na Wizara ya Tamisemi ikionyesha, takwimu za uachaji shule kwa wanafunzi nchini zimeongezeka karibia mara mbili zaidi mwaka 2017 ikilinganishwa na mwaka 2022, hali ni mbaya zaidi katika Wilaya ya Chamwino Kata ya Manzase ambapo takribani wanafunzi 170 wameacha shule ya sekondari ndani ya mwaka mmoja.

Idadi hiyo ya wanafunzi wanaoacha shule ni takribani asilimia 36.8 ya wanafunzi wote waliopo katika Shule ya Sekondari Manzase.

Wanafunzi hao wa ngazi ya Sekondari katika Vijiji vya Ilewelo, Sasajila na Kazaroho katika Kata ya Manzase wameacha shule mwaka 2023 sababu ikitajwa kuwa ni umbali wa kuifikia Shule ya Sekondari ya Manzase ambayo wanafunzi wa vijiji hivyo huitumia katika kupata elimu.

Ili wanafunzi wanaoishi katika Kijiji cha Kazaroho wafike shuleni hapo huwalazimu kutembea umbali wa kilomita 33, wanaotoka Ilewelo hutembea Kilomita 22 na wanaotoka Sasajila hutembea kilomita 10 kwenda Shule ya Sekondari ya Kata ya Manzase.

Akizungumza na Mwananchi Digital Diwani wa Kata ya Manzase, John Mika anasema baada ya uchunguzi wa matukio hayo ya wanafunzi wengi kuacha shule waligundua sababu ambayo ni umbali mrefu kuifikia shule.

Hata hivyo, Mika anasema barabara inayotumiwa kwenda umbali huo sio rafiki hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi hasa wa kike na kidato cha kwanza.

Baada ya matukio hayo Diwani Mika anaeleza kuwa wameweka mkakati wa kushirikiana na wananchi na viongozi wa vijiji kutoa elimu kwa watoto wao na kuwasihi waendelee na masomo.

“Kutokana na hali hiyo tunashirikiana na viongozi, walimu na wazazi kuwarudisha shuleni kwa kuwapa maarifa ya umuhimu wa elimu na kuna baadhi wenye changamoto sugu tunajaribu kushirikishana kuona namna ya kuzitatua,”alisema Mika.

Hata hivyo kiongozi huyo alisema licha ya changamoto ya umbali bado wanakumbana na hali ya wazazi wengi kutojua umuhimu wa elimu hivyo kushindwa kuwafuatilia watoto wao na kuwakatisha tamaa.

Mika alisema changamoto hiyo inawakumba zaidi kwasababu shule hiyo haina mfumo wa bweni hivyo wanafunzi wengi hukata tamaa na kuishia njiani.

“Ni changamoto na kama unavyojua shule zetu hazina mabweni na wanafunzi wanakutana na vishawishi huko na hivyo kutoroka, ingekuwa kuna mabweni yamekaa sehemu moja kidogo tunaweza kuwalinda na kuwafuatilia kwa karibu”alisema Mika.

Mratibu wa Elimu Kata ya Manzase, Leodgard Mosha alithibitisha kuwapo kwa umbali huo na kueleza ni ngumu kwa watoto kwenda shule kila siku hali inayosababisha utoro sugu kwenye shule hiyo yenye wanafunzi 462.

Mosha alisema kutokana na umbali huo baadhi ya wanafunzi hulazimika kuhamia kwa ndugu zao wanaoishi katika Kijiji cha Manzase, kupanga vyumba na wasio na uwezo wa hayo basi hujikuta wanaacha masomo.

Pia Mosha anasema kupitia nguvu ya wananchi sasa wameanza ujenzi wa shule nyingine katika kijiji cha sasajila ambapo watoto wa kijiji hicho na Ilewelo watasoma hapo.

Aidha katika hatua nyingine, Mosha amesema Serikali imeanzisha shule katika Kata ya Chiboli inayopakana na kata hiyo, hivyo wanafunzi wa Ilewelo watakuwa na unafuu wa kufika shuleni hapo.

“Mwanafunzi hawezi kutoka Ilewelo wala Sasajila akatembea kwa mguu akaja Manzase sekondari kwahiyo kwa asilimia kubwa wanaishi kwa ndugu zao waliopo Manzase lakini wengine wanalazimika kupanga kuondoa umbali”alisema Mosha.

Akizungumzia kuhusu wanafunzi kuacha shule, Mwenyekiti wa kijiji cha Manzase Charles Kangwe anasema wanafunzi wengi wanaishi katika nyumba zao binafsi ‘gheto’ kutokana na umbali huo hivyo kushindwa kujilinda na kuingia katika makundi yasiyofaa na hatimaye kuacha shule.

Kangwe anabainisha kama viongozi huwa na utaratibu wa kuwafuatilia watoto wanaosoma mbali kama wamefika shule na kwa ambao hawajafika hufuatiliwa kujua wana changamoto za aina gani.

Mkazi wa Kijiji hicho, Maria Thomas kuhusu changamoto hiyo anasema watoto wa vijiji ambavyo havina shule wanaathirika na umbali huo.

“Changamoto inayosababisha watoto waache shule ni umbali wa kuifikia pamoja na Korongo wanalokutana nalo njiani wakati wakiwa wanaenda shule,”anasema.

Katika njia ya kupambana na utoro shuleni kwa wanafunzi wa vijiji hivyo, Diwani Mika anasema kila siku katika mikutano ya vijiji na kata huelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa elimu na kuwasaidia watoto wao kujiendeleza hususan wa kidato cha kwanza na cha pili ambao ndio huacha kwa Idadi kubwa.

Wakati huohuo Mika alisema katika kijiji cha Kazaroho pia hakuna shule ya msingi hivyo kuwalazimu wazazi na viongozi kuchanga fedha kwaajili ya ujenzi wa madarasa ambayo sasa yapo katika hatua ya kupaua.

Kwa upande wa shule hiyo Mika alisema watoto wa chekechea, darasa la kwanza hadi la pili wanasoma katika majengo hayo ‘mapagare’ ili kuepuka umbali wa kufuata shule katika Kijiji cha Ilewelo ambapo ni umbali wa Kilomita 10 kwa mguu.

Takwimu za uachaji shule

Ripoti ya BEST 2022 inayotolewa na Wizara ya Tamisemi inasema; “Jumla ya wanafunzi 329,918 waliacha shule nchini mwaka 2022, kati yao wavulana ni asilimia 55.2 huku mwaka 2017 walioacha shule walikuwa 131,842 sawa na ongezeko la asilimia 150 (karibia zaidi ya mara mbili),”inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Ambapo ripoti hiyo pia inasema walioacha shule ya msingi walikuwa 193,605 mwaka 2022 wakiongezeka kutoka 66,142 mwaka 2017 na kwa upande wa sekondari walikuwa 136,313 mwaka 2022 wakiongezeka kutoka 65,700 mwaka 2017.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live