Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Thomas Mollel maarufu Askofu afariki dunia

Tue, 21 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mfanyabiashara maarufu wa madini nchini Tanzania, Thomas Mollel maarufu kwa jina la Askofu amefariki dunia jana usiku Jumatatu Mei 20, 2019  jijini Dodoma.

Alikwenda Dodoma kushuhudia kuapishwa kwa mbunge mteule wa Arumeru Mashariki (CCM),  Dk John Pallangyo.

Mollel ambaye mwaka 1995 alipata umaarufu baada ya kugawa fedha akiwa ghorofani huku wananchi wakiziokota chini, amefariki dunia saa tano usiku, muda mfupi baada ya kutoka kuoga akiwa na mkewe.

Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Meru, Joshua Hungura amesema kabla ya kifo chake, Mollel alikuwa mzima na jana saa nne usiku walikula pamoja chakula cha jioni.

Amesema Mollel ambaye pia alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM Wilaya ya Meru na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya wilaya hiyo,  siku za nyuma alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu.

"Lakini tulitoka salama Arusha alikuwa mzima kabisa akifurahia kuja kuapishwa mbunge wetu na alifariki ghafla akiwa ametoka kuoga baada ya kudondoka mlangoni,” amesema Mollel.

Pia Soma

Amesema mwili wa Mollel unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda Arusha baada ya Pallangyo kuapishwa.

"Tumeshauriana ni vyema sote kama tulivyokuja turudi na mwili wa mpendwa wetu na taratibu za mazishi zitatolewa baadaye,” amesisitiza.

Enzi za uhai wake, Mollel alikuwa pia mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite na aliwahi kumiliki timu ya mpira wa miguu ya Pallson iliyowahi kushiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Pia, amewahi kuwa diwani wa Mbughuni.

Chanzo: mwananchi.co.tz