Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tetemeko la ardhi la 4.7 latikisa Mara

7a88338d3df7b5db09e91ca4509821d6 Tetemeko la ardhi la 4.7 latikisa Mara

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TETEMEKO la ardhi limesababisha taharuki mkoani Mara lakini hakuna madhara makubwa kwa binadamu.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima jana alithibitisha kutokea kwa tetemeko hilo alipozungumza na HabariLeo jana kwa simu.

Kamanda wa Polisi wa Mara (anayesimamia wilaya nne), Daniel Shilla, alilieleza HabariLEO kuwa, tetemeko lilitokea jana saa 10:48 alfajiri na lilidumu kwa dakika mbili.

"Ni kweli nimepokea taarifa kwamba katika eneo langu yaani wilaya nne; Serengeti, Bunda, Butiama na Manispaa ya Musoma kumetokea tetemeko lakini mpaka sasa hakuna madhara kwa binadamu wala mali," alisema Kamanda Shilla.

Kwa mujibu a taarifa za kijiolojia tetemeko hilo lililosikika pia Kenya lilitokea kilomita 45 kutoka Musoma na lilikuwa na nguvu ya magnitude 4.7 majira ya alfajiri saa 10.47, kikiwa na kina cha kilomita 10.

Kamanda huyo alisema anaamini kuwa hali za watu ni salama kwa kuwa mpaka jana mchana hapakuwa na taarifa za majeruhi wala mali kuharibiwa kwa tetemeko hilo.

"Tuna askari mpaka ngazi za vijiji na kata, kungekuwa na madhara yoyote taarifa tungeshapata, tunaamini wananchi wapo salama. Ila kama kuna madhara yoyote watoe taarifa," alisema Kamanda Shilla.

Septemba 2016 lilitokea tetemeko wilayani Bukoba, mkoani Kagera na kusababisha maafa kwa vifo kadhaa na uharibifu wa majengo zikiwemo nyumba za makazi na shule.

Aidha matetemeko yasiyo na madhara yameripotiwa mara kadhaa katika mikoa mbalimbali nchini likiwemo la mwaka jana, jijini Dar es Salaam.

Chanzo: www.habarileo.co.tz