Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tembo waua sita Makuyuni

Bd0812800b319275c15be9c539b50acc Tembo waua sita Makuyuni

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TEMBO wameua wananchi sita na kujeruhi wengine saba katika Kijiji Cha Makuyuni Wilaya ya Monduli mkoani Arusha katika kipindi cha miaka miwili.

Aidha tembo hao wanadaiwa kuvamia pia mashamba ya wananchi na kuharibu mazao, hivyo kusababisha wakose chakula na kuishi maisha ya tabu. Mwenyekiti wa Kijiji Cha Makuyuni, Ngayoo Measi aliyasema hayo wakati wa mazishi ya mkazi mmoja, Ester Sindiyo (55) aliyeuawa na tembo Desemba 21 mwaka huu akiokota kuni.

Alisema, makundi ya wanyama hao wanaotoroka kutoka hifadhi za taifa za Tarangire na Manyara, hutembea kijijini hapo kutafuta malisho nyakati za usiku na hakuna jitihada zinazochukuliwa kuwadhibiti. Mwenyekiti huyo alitaja watu waliouawa na tembo kwa nyakati tofauti kuwa ni Janeth Silla, Mamalai Kakuyu, Lemomo Lenguriny, Kastuli Jumalei, Emanuel Leroo na Ester Sindiyo, wote wakazi wa kijiji hicho.

Aliwataja waliojeruhiwa na tembo hao ni Lobulu Mollel, Julius Thobias, Saiguran Mika, Mnyak Lenguriny na Mjomba Soingei ambaye bado amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Lobikyeki Sanare na Kalai Lomayani. Wote ni wakazi wa kijiji hicho.

Taarifa za matukio hayo wamekuwa wakizitoa katika ngazi mbalimbali. Diwani wa kata hiyo, Elius Odupoi aliwataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujilinda na wasitembee au kufanya shughuli za kijamii usiku.

Mmoja ya wakazi wa kijiji hicho, Peter Laisangai aliiomba serikali kuongeza fidia kwa waathirika wa wanyamapori, kwa kuwa kiasi kinachotolewa na serikali cha Sh 500,000 kwa aliyejeruhiwa na Sh 1,000,000 kwa aliyefariki dunia ni kidogo .

“Tunaiomba serikali kupitia upya kiasi kinachotolewa kama kifuta jasho kwa waathirika wa wanyamapori kwani hakiendani na thamani ya mwananchi anayelinda rasilimali hizo”alisema Laisangai Ofisa Wanyamapori Wilaya ya Monduli, Seraphino Mawanja alisema kwenye mazishi hayo kuwa katika kipindi cha miaka miwili maeneo hayo yamekuwa na changamoto kubwa ya ongezeko la tembo kutoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

Tembo hao huhama baada ya mvua nyingi kunyesha na maeneo yao kujaa maji. Alisema serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa kuwaondoa tembo hao wanaovamia maeneo ya makazi kwa kuweka askari wa doria.

Chanzo: habarileo.co.tz