Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tembo watishia amani wakazi wilayani Mwanga

112252 Tembo+pic

Sun, 8 Nov 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanga. Tembo waliovamia katika maeneo ya makazi ya watu katika tarafa ya Jipendee, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wamesababisha baadhi ya wananchi kuhofia kutoka nyumbani kwenda kwenye shughuli za uzalishaji mali, huku wanafunzi nao wakihofia kwenda shule.

Tembo hao wameshafanya uharibifu katika kata tano za tarafa hiyo, ambazo ni Kwakoa, Toloha, Kigonigoni, Jipe na Kivisini, huku zilizoathirika zaidi zikiwa ni kata ya Kwakoa na Toloha ambazo zimepakana na Hifadhi ya Tsavo nchini Kenya na Mkomazi iliyopo Wilaya ya Same.

Oktoba 31, 2020 aliyekuwa mwalimu wa kujitolea katika shule ya sekondari Kwangu, Rojas Willison, alifariki dunia baada ya kushambuliwa na tembo alipokuwa akitoka kutafuta mahitaji.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, mwalimu mkuu shule ya msingi Kwakoa, Emmanuel Kilawe na diwani wa kata ya Kwakoa, Kiende Mvungi, wameelezea namna tembo hao walivyoongezeka na kuonekana katika maeneo ya makazi ya watu nyakati za asubuhi na mchana tofauti na awali ambapo walizoeleka kupita usiku.

Kufuatia hali hiyo, wameiomba Serikali kuona namna ya kuwafukuza na kuwarudisha katika eneo la hifadhi,ili kuwezesha wanafunzi kwenda shule na jamii kuendelea na shughuli za uzalishaji mali kwa amani.

Mvungi, alisema tembo wamekuwa wakiongezeka na kuonekana wakipita mitaani hadi mchana na si usiku tena kama ilivyokuwa zamani.

Pia Soma

Advertisement
“Kwa sasa presha ya tembo imekuwa kubwa, maana wamekuwa wakiingia maeneo ya watu asubuhi,mchana na hata jioni tofauti na hapo nyuma ambapo walikuwa wakionekana usiku na ilikuwa rahisi watu kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha wanarudi nyumbani mapema,”alisema.

“Lakini wapo watoto wanatoka umbali wa kilometa nne kutoka nyumbani hadi shule ya msingi Kwakoa na sasa hawaendi shule kila siku kutokana na wazazi wao kuhofia tembo kwa kuwa watoto hao huwa wanaondoka nyumbani mapema alfajiri ili kuwahi shule,”aliongeza.

Aidha, alisema ipo haja sasa ya Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, kuona namna bora ya kuwafukuza tembo hao katika maeneo ya makazi ya watu na kuwarudisha hifadhini pamoja na kuangalia uwezekano wa kujenga uzio wa umeme ili kuwadhibiti kutoka ndani ya eneo la hifadhi.

Mwalimu mkuu shule ya msingi Kwakoa, Emmanuel Kilawe, alisema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni hofu, ambayo imesababisha baadhi ya wanafunzi kufika shule saa mbili, jambo ambalo limekuwa likiathiri masomo yao.

“Hofu imetawala, na sasa kuna wakati tembo wanakatiza maeneo ya shule muda wa saa mbili mpaka saa tatu asubuhi,hali ambayo inaibua hofu kubwa, lakini pia hofu hii imesababisha utoro wa rejareja.”

“Naiomba Serikali isaidie kupambana na hili tatizo ili kuona namna ya kuondoa tembo hao katika makazi ya watu kwa kuwa siyo wanafunzi tuu wenye hofu, jamii nzima inawahofia wanyama hawa. Jitihada zifanyike kuhakikisha wanawarudishwa kwenye maeneo yao ya hifadhi,’’ alieleza.

Kamishna msaidizi wa uhifadhi, Hifadhi ya Taifa Mkomazi Emanuel Moirana, alikiri tembo kuongezeka na kusema wameendelea kupambana na wanyama hao, ili kuwarudisha hifadhini na kuhakikisha athari zinapungua kwa mazao na mali za wananchi.

“Tumeendelea kushirikiana na wananchi kufukuza wanyama hao, lakini pia tayari tumetoa vifaa kama tochi za usiku kwa ajili ya kufukuza wanyama hao pamoja na vuvuzela ikiwa ni moja ya mikakati ya kuwadhibiti”

Alisema kwa sasa wameanza na tochi nne na vuvuzela nane katika kijiji cha Ngulu na wanajipanga pia kupeleka kijiji cha Kwakoa Vvvuzela nyingine 12 na tochi nne.

Alisema pia wanaendelea na mikutano ya wananchi kwa ajili ya kutoa elimu na kushirikiana nao kuwafukuza wanyama hao, ili warudi kwenye hifadhi na wanaamini baada ya muda hali itakuwa nzuri.

Alisema chanzo cha wanyama hao kuongezeka katika kipindi hiki ni kutokana na maeneo hayo kuwa mapitio ya wanyama na ambayo wanyama wanatawanyikia.

“Lakini pia, mwaka huu kumekuwa na ukame mkubwa ambao umesababisha maji kwenye maeneo ya uhifadhi kukauka na malisho kupungua, hivyo wanyama hao wanaondoka kutafuta malisho na maji,”alisema Moirana na kuitaka jamii kuchukua tahadhari.

Chanzo: mwananchi.co.tz