Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tembo, tumbili walalamikiwa kuingia katika makazi ya watu

34650 Tembo+pic Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uwepo wa wanyama wengi katika hifadhi mbalimbali nchini, unachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii kutoka nje ya nchi kuja kutembelea mbuga na hifadhi hizo.

Hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa hifadhi husika na Taifa kwa ujumla kupata fedha za kigeni kupitia watalii kisha fedha hizo kutumika katika maendeleo.

Hata hivyo, uwepo wa hifadhi wakati mwingine unaweza kuwa kero kwa wanavijiji wanaoishi jirani, kwa kuwa wanyama hasa tembo wamekuwa wakitoka hifadhini na kwenda katika makazi ya watu.

Hali hiyo inawakumba mara kwa mara wakazi wa vijiji vilivyo jirani na hifadhi mbalimbali kama ilivyo kwa vijiji vya King’ori na Ngong’ongare vilivyopo wilayani Arumeru vinavyozungukwa na Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Anapa).

Wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakikumbana na tembo na tumbili wanaoingia katika makazi yao.

Oktoba mwaka huu Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID-Protect), likishirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kuwapa mafunzo ya namna ya kuripoti habari za uhifadhi wa mazingira na wanyamapori na kuwawezesha kutembelea hifadhi na kuzungumza na wananchi.

Wakizungumza na gazeti hili kuhusu uhusiano kati yao na Anapa na changamoto zinazowakabili, baadhi ya wananchi wanasema uwepo wa wanyama wengi una manufaa kwao kwa kuwa unafanikisha kupatikana fedha zinazotumika katika miradi ya maendeleo.

“Anapa wanatusaidia kuboresha maendeleo hapa kijijini. Hii inatokana na ushirikiano uliopo kati yetu na wao. Tumefanikiwa kudhibiti ujangili na kuimarisha utunzaji wa mazingira yanayochangia kuongezeka kwa wanyama.

“Tatizo tunalolipata mara kwa mara ni tembo kuja kwenye makazi yetu. Ni kweli tunafurahia ongezeko lao hifadhini lakini wamekuwa wakitubughudhi kiasi kwamba tunashindwa kufanya shughuli za maendeleo ikiwamo kilimo,” anasema Charles Kitambaa mkazi wa Ngong’ongare.

Kitambaa anasema tembo wanaokwenda katika makazi yao wamegawanyika katika makundi matatu; kwanza, linaloongozwa na mwenye jino moja, la pili wanatembea wanne na la mwisho wanatembea watatu.

“Tunakutana na tembo hawa mara kwa mara lakini hatuwezi kuwadhuru kwa sababu ya uhusiano wetu na Anapa. Tukiwajeruhi nafsi zitatusuta kwa namna hifadhi hii inavyosaidia kuboresha miradi ya maendeleo katika vijiji vinavyoizunguuka,” anasema.

Hata hivyo, Kitambaa aliipongeza Anapa chini ya Mhafadhi Mkuu Steria Ndaga kwa kuwa mstari wa mbele kutoa ushirikiano haraka pindi wanapopata taarifa kuwa tembo wametoka nje ya hifadhi hiyo.

Mbali na tembo, Kitambaa anasema kumekuwa na kundi la tumbili wanaokwenda kwenye makazi yao, kutafuta chakula na wanapokikuta hata kama ni ndani ya nyumba huchukua na kuondoka navyo.

“Hawa ndiyo shida zaidi kwetu, maana wakifika nyumbani kwako wanakwenda moja kwa moja hadi jikoni na kuchukua vyakula vinavyopikwa hata kama ni vya moto. Wamekuwa wasumbufu na wanakuja wengi sana,” anasema Kitambaa.

Naye Joshua Mbise anasema kuvamiwa na tembo hao mara kwa mara katika makazi yao kunawanyima fursa ya kufanya shughuli za maendeleo ikiwamo kilimo kwa kuhofia mazao yataharibiwa.

Kutokana na hali hiyo, Mbise ameiomba Anapa kuweka utaratibu maalumu utakaowadhibiti wanyama kutoka mara kwa mara katika hifadhi hiyo kwenda kwenye makazi yao.

Kauli ya DC

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Arumeru, Jerry Muro ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, anakiri kuwapo kwa changamoto katika hifadhi hiyo yenye ukubwa wa mita za mraba 322 ikijumuisha Mlima Meru wenye urefu wa mita 4,566 kutoka usawa wa bahari.

Anasema sababu mojawapo ya changamoto hiyo ni kutokana na ardhi kutoongezeka huku wananchi wakiongezeka. “Hifadhi haiongezeki ndio maana wanyama wamekuwa wakisogea hadi maeneo ya makazi. Tutaendelea kushirikiana kuwadhiti bila kuharibu utalii wetu”.

Tawa

Ofisa Habari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) Twaha Twalib anasema kuongezeka kwa tembo katika hifadhi hiyo ni matokeo ya kudhibiti ujangili na kujenga uelewa kwa wananchi.



Chanzo: mwananchi.co.tz