Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tembo kulelewa kituo cha yatima

50400 TEMBO+PIC

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha, Kama ulikuwa unadhani, vituo vya yatima na wanaoishi katika mazingira magumu vipo kwa binadamu basi unakosea, kwani sasa vimeanzishwa vituo vya kulea wanyama yatima ambao wapo hatarini kutoweka duniani.

Makao Farm ni moja ya vituo hivi, kipo Moshi mkoani Kilimanjaro na kituo kingine kipo West Kilimanjaro, mkoani Kilimanjaro vituo hivi vinaendeshwa na wadau wa uhifadhi chini ya uangalizi wa Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA).

Wanyama ambao wanatunzwa katika vituo hivi ni wale ambao maisha yao yapo hatarini na baada ya kufikia umri wa kuweza kujimudu porini huachiwa kuingia porini kuendelea na maisha yao.

Hivi karibuni, kituo hicho cha Makoa kilipata tembo mmoja wa kumlea ambaye aliokolewa akiwa ametumbukia korongoni.

Tembo huyu mtoto mwenye umri kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja alisafirishwa kwa ndege ya taasisi ya uhifadhi ya Friedkin Conservation Fund (FCF), baada ya kukutwa na askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) akiwa korongoni jirani na pori la akiba la Lwafi katika Kijiji cha China, mkoani Katavi.

Safari ya kumsafirisha

Safari ya kuokoa maisha ya tembo huyo kutoka Sumbawanga hadi Moshi, ilichukuwa saa tatu angani na kugharimu zaidi ya Sh20 milioni.

Tembo huyo alisafirishwa kwa ndege ya watalii shirika la Northen Air, mali ya taasisi ya Friedkin, kutoka uwanja wa ndege wa Sumbawanga hadi uwanja mdogo wa ndege wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mtoto huyu wa Tembo alisafirishwa huku akiwa anachomwa sindano za usingizi kila baada ya muda ililazimu kumshika miguu yake kwa nguvu ili asilete madhara ndani ya ndege kila ganzi ilipoisha.

Ndege iliyombeba iliyokuwa na watu wanne akiwamo mwandishi wa makala hii na marubani wawili, inawezekana ikawa ni miongoni mwa safari ngumu iliyofanikiwa kuokoa maisha ya mnyama huyu ambaye thamani yake ni zaidi ya 33 milioni.

Kazi ya kumpakia kwenye ndege tembo huyu haikuwa ndogo, kwani ililazimu zaidi ya askari 5 na wahifadhi wanne kushiriki kumbeba na kumpakia.

Akiwa angani, tembo huyu alipatiwa huduma za afya kama binadamu ambaye anasafirishwa kupelekwa hospitali kubwa, kwani licha ya kupewa dawa za usingizi, alipewa tiba ya majeraha aliyopata na alisaidiwa kupata hewa safi.

Waliosafiri na mnyama huyo ya ndege, walilazimika kumshika miguu, kumtuliza kila ganzi ilipompungua na kujaribu kuinuka.

Maisha yake akiwa kituoni

Tembo huyo akiwa chini ya uangalizi maalumu, alifika kituo cha yatima cha Makoa Farm na kutokana na umri mdogo wa chini ya mwaka mmoja analazimika kuishi kwa kunywa maziwa.

Kamishna Mkuu wa TAWA, Dk James Wakibara akizungumza baada ya kumtembelea tembo huyo anasema maisha yake yanaendelea vizuri na anakunywa maziwa huku akipewa matibabu.

Dk Wakibara anasema mtoto huyo wa tembo kwa siku anakunywa kati ya lita 11 hadi 17 za maziwa huku akiendelea kupata matibabu mengine ili baadaye aweze kujitegemea kula vyakula vya kawaida. “Anapewa maziwa kwa sababu pia alipata majeraha mdomoni hivyo imekuwa ni vigumu kwake kula kama kawaida,” anasema.

Anasema suala la vituo vya kulea wanyama yatima ni jambo geni hapa nchini, lakini ni muhimu hasa kwa wanyama ambao maisha yao yanakuwa hatarini baada ya wazazi wao kupotea au kufa.

Kamishna Wakibara anasema nia ya TAWA na Wizara ya Maliasili ni kuwa na vituo vyake ya kulea wanyama wadogo walio hatarini kutoweka duniani ili kuendeleza uzao wao.



Chanzo: mwananchi.co.tz