Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Teknolojia, bodaboda vinachangia mimba kwa wanafunzi

42105 Atharipic Teknolojia, bodaboda vinachangia mimba kwa wanafunzi

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya wazazi na walezi wamesema mazingira magumu ya kusomea na kukua kwa sayansi na teknolojia ni sababu kubwa ya wanafunzi wengi kukatisha masomo kwa mimba.

Wazazi hao wamesema vijana wengi hawapati shida kuwanasa watoto wa kike kutokana na uwepo wa simu za mkononi na usafiri wa bodaboda.

Wakizungumza katika kampeni ya kutokomeza tatizo hilo inayoendeshwa na shirika linalojishughulisha na masuala ya kisaikolojia kwa watoto (Repssi), kwenye vijiwe vilivyo katika mitaa na vijiji vya kando ya barabara ya Kilwa leo Februari 16, 2018.

Mkazi wa kijiji cha Bungu B, Shaban Ramadhan amesema wanafunzi wengi wanamiliki simu za mkononi kinyemela hivyo kurahisisha mawasiliano baina yao na vijana wakiwamo bodaboda ambao huwapa lifti kwenda na kurudi shule kutokana na umbali mrefu kutoka kwenye makazi yao mpaka shuleni.

“Fikiria shule ipo kilomita mbili mpaka 10, huyu msichana anaweza kutembea kila siku na kuhimili vishawishi vya njiani? Wazazi tusilaumiwe peke yetu mazingira ya watoto huko shuleni hayako sawa,” anasema.

Awali mkurugenzi mkazi wa Repssi, Edwick Mapalala alisema wazazi wanayo nafasi kubwa katika kuchangia mafanikio ya vita dhidi ya mimba shuleni.

Amesema wazazi na walezi wanawajua wahusika waliowapa mimba watoto wao lakini huwa wanamalizana kifamilia na kukaa kimya.

Amesema wazazi hao hukubaliana kwamba kama mtoto wa kike atapewa matunzo yote na kijana aliyempa mimba basi hakuna shida yoyote.

“Hii vita haitamalizika licha ya kuwepo kwa sheria na harakati za kumalizana na tatizo hili kama wazazi na walezi hawatatoa ushirikiano, badala ya kulaumu na kutoa sababu, tusaidiane kwenye hili kwa sababu si tu kwamba athari ya mimba za utotoni ni kukatisha masomo au kuhatarisha afya ya mtoto hata kisaikolojia mtoto anaathirika kwa kiasi kikubwa,” amesema Mapalala.

Amewashauri wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika maadili na kutosita kuzungumza nao masuala yahusuyo afya ya uzazi.

“Msikae kimya na mkiona kijana hana muenendo mzuri kwa watoto wa kike kijijini, mkanyeni na ikiwezekana mkamshitaki ili asiendele, hatuwezi kufikia ndoto ya Tanzania ya viwanda kama mamia ya watoto wa kike Tanzani watakua wanakatisha masomo kwa mimba,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz