Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tehama kuleta mabadiliko Bandari Mtwara

B7c23fa88c61ccac33e9cc02d8c6c094 Maboresho Mfumo wa Tehama

Tue, 3 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia mzigo wake katika Bandari ya Mtwara kutoka ughaibuni, sasa anaweza kufanya hivyo akiwa nyumbani au ofisini kwake bila kulazimika kwenda bandarini.

Hatua hiyo inatokana na maboresho makubwa ya mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambayo yamekuwa yakifanywa mara kwa mara na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika kuboresha utendaji na ufanisi katika bandari hiyo, anasema Khalfan Yakubu, Ofisa Tehama wa bandari ya Mtwara.

Anafafanua kwamba kupitia Tehama mteja sasa anaweza kutengeneza bili yake, akafanya malipo na kila kitu huko aliko na mambo yote yakaenda sawa, tena ndani ya dakika chache tu.

Ameongeza kusema kwamba wanayo mifumo kadhaa ya Tehama na kwa kupitia mfumo tendaji (operation) uliogawanyika katika mifumo mingine mitatu midogo ndio unaosababisha shughuli nyingi za bandari ya Mtwara kwenda kwa wepesi katika kuhudumia wateja.

Anaitaja mifumo hiyo midogo kuwa ni unaohusu kupokea na kushusha mizigo (cargo system), mfumo wa kupokea maelezo ya mzigo (bill system) na mfumo wa malipo (integrated electronic payment system - IEPS).

Mtalaamu huyo wa Tehama anasema baada ya mteja kukamilisha masuala ya kutuma au kupokea mzigo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa maana ya kulipa kodi, ndipo sasa huanza kushughulika na bandari tayari kwa kuleta au kupokea mzigo wake.

Anasema habari zake huwemo pia kwenye mfumo wa Tehama wa TRA unaojulikana kama Tanzania Customs Integrated System (Tancis).

“Pamoja na kwamba hata sisi tutaona taarifa zake kwenye Tancis kwa sababu tumeunganishwa na huo mfumo, mteja atakuja kwenye mifumo yetu ili kutoa taarifa ambazo zitatuwezesha kuanza kumshughulikia.

“Ataeleza aina ya mzigo wake na taarifa kuhusu meli kwa maana ya urefu na uwezo wake na lini inatarajiwa kufika au kuondoka,” anasema.

Anasema kwamba taarifa hizo ni muhimu kwani huisaidia bandari kujipanga vyema katika kuhudumia meli husika kwa ufanisi na kwa haraka ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau muhimu.

Anatoa mfano kwamba kama mzigo unahusu mionzi inapaswa wawepo wataalamu wa nguvu za atomiki ili kutoa ushauri wa kitaalamu.

Anasema pamoja na mteja kueleza taarifa kuhusu meli, huwa pia wanazithibitisha ukweli wake kupitia taarifa za Wakala wa Umoja wa Mataifa unaohusika na udhibiti na usajili wa meli (International Maritime Organization - IMO).

Usahihi wa taarifa ukishathibitishwa, anasema Yakubu, watu wa Kitengo cha Mapato huanza kumtengenezea mteja tozo za awali.

Anataja tozo hizo kuwa ni pamoja na tozo za kuingiza meli bandarini, tozo za kufunga meli na tozo zingine za bandarini. Akielezea namna meli inavyoingia bandarini, Mkuu wa Idara ya Ubaharia, Shaban Kassimu Abdi, anasema meli ikishaingia katika eneo la bandari, wanaifuata na nahodha wao hadi kuifunga kwenye gati na kwamba muda wote wanakuwa wanaiongoza kuingia gatini kwa kutumilia mlingoti wa kuongozea meli.

“Meli ni kama gari. Kama unajua kuendesha gari basi gari lolote unaweza kuendesha, kwa hiyo (kutokana na sheria za kimataifa) sisi ndio tunaingiza meli gatini,” anasema nahodha huyo.

Yakubu anafafanua kwamba mteja anayetaka kutuma mzigo anapaswa kwanza awe na wakala wa meli (shipping agent) ambaye atahusika na kumtafutia mteja usafiri (meli) na pili awe na wakala wa forodha (clearing and forwarding agent) atakayeshughulikia utoaji wa bidhaa zake bandarini kwa sababu bandari haishughuliki na mtu wala mfanyabiashara mmoja mmoja.

“Kimsingi wakala wa meli ndiye anashughulikia malipo au tozo za meli na shughuli zake huishia pale meli inapofungwa gatini na wakala wa forodha hushughulikia mambo yote yanayohusu utoaji wamzigo kwenye meli au kuuingiza melini,”

Anasema tozo za meli na namna ya kuzihudumia hutofautiana kati ya zile zilizosajiliwa Tanzania na kufanya kazi katika eneo hili la Afrika Mashariki na zile ambazo hazijasajiliwa nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz