MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) inatarajia kuandaa mpangokazi utakaowezesha kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi karibu na mapori ya akiba ya wanyamapori, ukiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kusimamia utatuzi wa migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.
Mkakati huo wa kitaifa ulizinduliwa Oktoba 8, 2020 jijini Dodoma na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla.
Kaimu Kamishna wa Tawa, Mabula Nyanda, alisema hayo juzi wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha menejimenti ya mamlaka hiyo kilichofanyika mkoani Morogoro.
Nyanda alisema tatizo la mgongano wa binadamu na wanyama kwenye maeneo ya hifadhi yanayozungukwa na wananchi ni kubwa na kutokuwepo kwa takwimu kamili, lakini zaidi ya watu 50 wanapoteza maisha kila mwaka na karibu ekari 5,000 za mazao mbalimbali huharibiwa nchini kote.
Alisema katika kutafuta suluhu endelevu na kwa kuzingatia umuhimu wa kutatua changamoto ya migongano kati ya wanyamapori na binadamu, Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa mkakati wa kitaifa wa kusimamia utatuzi wa migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.
"Tawa imeona ni muhimu kuweka mikakati ya kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi pambezoni kuzunguka mapori ya akiba ya wanyamapori na elimu hii italenga jinsi wananchi wajiepushe na wanyama hao wakiwemo tembo na simba ambao mara nyingi wamekuwa wakiripotiwa kuleta mgongano baina yao na binadamu," alisema.
Mkakati huo unalenga kuwezesha jamii kutumia mbinu shirikishi na zisizokuwa na madhara kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, ikiwa na kupunguza madhara ya kuishi na wanyamapori.
Lengo lingine ni kuongeza uwezo wa wizara kukabiliana na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, na kuhimiza matumizi bora ya ardhi, hasa katika maeneo ya shoroba na yenye mtawanyiko wa wanyamapori.