Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo la usafiri lahamia Moshi, nauli za kurejea D’Salaam zapaa

34308 Pic+moshi Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Licha ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), kuwaonya wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwa wasipandishe nauli, bei ya tiketi mjini hapa imepanda na kuibua malalamiko kutoka kwa abiria.

Jana asubuhi katika Stendi Kuu ya Mabasi Moshi, kulikuwa na msongamano wa watu waliokuwa wakisaka usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali, hususan Dar es Salaam lakini wengi walikwama kutokana na nauli kupanda ghafla hivyo kushindwa kumudu.

Walikuwa wakitozwa kati ya Sh35,000 hadi Sh40,000 kwa mabasi yaliyokuwa yakienda Dar es Salaam badala ya kati ya Sh25,000 na Sh32,800.

Mwananchi lilizungumza na baadhi ya abiria hao kuhusu kupanda kwa nauli ambao walisema licha ya kutozwa nauli hiyo isiyo halali, tiketi zao zilikuwa zinaandikwa Sh25,000.

Abiria hao walieleza kushangazwa na ongezeko la nauli na kuzitaka mamlaka husika kushughulikia suala hilo haraka kwani walinawaumiza wanyonge.

Anitha Anselim, aliyekuwa akisafiri kwenda Dar es Salaam, alisema alipofika stendi alikuta msongamano huo kuhu wakatisha tiketi wakiwatangazia nauli kubwa badala ya ile iliyowekwa kisheria.

“Watu ni wengi mno, ndiyo maana hawa wenye mabasi wanaringa, wanapandisha nauli ovyo, kiukweli tunaumia kwa hizi gharama,” alisema Anitha.

“Nimekuja hapa na ndugu zangu wawili nikiwa na Sh75,000 nashangaa ninaambiwa nauli ni Sh40,000 (kwa mtu mmoja) tena kwa magari ambayo siyo ya luxury.”

Janeth Ngowi aliyekuwa akisafiri kwenda Arusha aliilalamikia Sumatra kwa kushindwa kudhibiti alioutaja kuwa ni uhuni wa makondakta wanaokatisha tiketi.

Alisema kama Sumatra wangekuwa makini kutekeleza majukumu yao, nauli zisingepanda kiholela. “Haiwezekani nauli kutoka Moshi mjini kwenda Arusha mtu anatozwa Sh5,000 badala ya Sh2,500 ambayo ni halali,” alisema Janeth.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Kilimanjaro, John’s Makwale alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo, alisema alishatoa taarifa kuwa abiria wanatakiwa kukata tiketi kwenye ofisi za mabasi na si kwingineko.

“Nimeshasema watu wakate tiketi ndani ya ofisi za mabasi ili waepukane na madalali,” alisema.

“Tunaendelea kuwasaka, watakapobainika wanatoza abiria nauli kubwa, tutawachukulia hatua na tunaomba ushirikiano wa abiria wanaosafiri pale wanapobaini wanapandishiwa nauli.”

Vilevile, aliwataka abiria kutoa ushirikiano utakaowezesha kukomesha tabia hiyo huku akiwasihi kutokubali kulipa nauli tofauti na iliyopitishwa kisheria.



Chanzo: mwananchi.co.tz