Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo la maji Mtwara Mikindani kutatuliwa

1ac9fcfc387fbb09f63e41a5d93360fd Tatizo la maji Mtwara Mikindani kutatuliwa

Fri, 25 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATUMIAJI wa maji katika Manispaa ya Mtwara Mikindani wametakiwa kuwa na uvumilivu kwa kipindi cha miezi sita wakati serikali ikifanyia marekebisho ya chujio katika kituo cha kuchujia maji kilichopo Mangamba (Mtawanya) ndani ya manispaa hiyo.

Akizungumza katika ziara ya kukagua miundombinu na miradi mbalimbali ya maji ndani ya manispaa hiyo hivi karibuni, Mkurugenzi wa Ubora wa Maji kutoka Wizara ya Maji, Philipo Chandy, alisema ndani ya miezi sita, wananchi hao watakuwa na uhakika wa kupata maji ya kutosha baada ya kukamilika kwa chujio hilo na kusambaza maji safi na salama tofauti na hali ilivyo sasa.

Alisema wizara hiyo ipo katika hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma na kuyasambaza katika maeneo yenye shida ya maji hususani wilaya ya Nanyumbu.

Chandy ambaye pia alikagua miradi ya maji ya Mtawanya, Mchuchu Mikindani, Mji Mwema na Lwelu alisema: “Maandalizi ya awali yameshakamilika hivyo tunatafuta fedha kwa ajili ya kutoa maji kutoka Mto Ruvuma na kuyapeleka Nanyumbu na maeneo yenye shida ya maji, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeondoa shida hii kwa Mtwara mzima,”alisema.

Akizungumzia upatikanaji wa maji mkoani humo, Meneja wa Maji wa Ruwasa, Mbaraka Rajabu, alisema upatikanaji wa maji ni asilimia 60.1 kwa vijijini na asilimia 85 kwa mjini.

Alisema sehemu kubwa ya maji hayo yanapatikana chini na juu ya ardhi, ambapo kwa mwaka lita milioni 11.7 hupatikana juu ya ardhi na matumizi hukisiwa kuwa ni lita milioni 2,000, ambayo ni sawa na asilimia 19.

Aidha, lita milioni 3300 za maji hupatikana chini ya ardhi na matumizi kukisiwa kuwa lita milioni 419 sawa na asilimia 12 zinazotumika kwa mwaka.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mtwara (Mtuwasa), inaendelea kujenga miradi mingine ya maji.

Takribani miradi 34 inatarajiwa kuanzishwa na kukamilishwa ndani ya mwaka huu na imepanga hadi kufikia Desemba, mwaka huu iwe imekamilika kwa asilimia 100.

Chanzo: habarileo.co.tz