Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo la maji Kigamboni kumalizika Aprili mwakani   

90cc257fb42a6bfbf72e22ccfe2aee1f Tatizo la maji Kigamboni kumalizika Aprili mwakani   

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TATIZO la maji katika Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam, linatarajiwa kumalizika mwezi Aprili mwakani, baada ya kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Kigamboni.

Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), unahusu uendeshaji wa visima vya maji vya Kimbiji wilayani Kigamboni na Mpera wilaya ya Mkuranga.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Dawasa, Davis Mwamunyange na wajumbe wa bodi hiyo, walitembelea mradi huo wa Kigamboni na Mradi wa Mkuranga mwishoni mwa wiki.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwamunyange alisema matatizo ya maji kwa wakazi wa Kigamboni na Mkuranga yatakwisha karibuni.

Alisema yeye na wajumbe wa bodi hiyo, wameridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo ya Kigamboni na Mkuranga.

“Kwa sasa ujenzi unaendelea katika hatua nzuri. Wakandarasi wanafanya kazi kwa kasi na kufikia Aprili mwaka 2021 wananchi wataanza kupata huduma ya majisafi” alisema.

Mwamunyange alisema “Mradi huu wa visima vya Kimbiji na Mpera ni moja ya miradi mikubwa sana. Mradi huu utamaliza tatizo la maji Kigamboni na Mkuranga na baadhi ya maeneo ya Temeke.”

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja alisema hadi sasa visima 14 vimechimbwa katika maeneo ya Kimbiji na Mpera, ambapo Kimbiji visima 11 na Mpera vitatu. Visima hivyo vina urefu wa mita 400 hadi 600.

Visima saba vilivyokamilika eneo la Kimbiji, vina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 57 kwa siku huku mahitaji ya wakazi wa Kigamboni ni lita milioni 25 tu za maji kwa siku.

Luhemeja alisema wananchi wa Kigamboni wategemee kupata huduma ya majisafi ifikapo mwezi Aprili mwakani na maeneo yatakayonufaika ni Kibada, Toangoma, Kigamboni, Mjimwema, Vijibweni, Kimbiji, Kisarawe Two na Gezaulole.

Kwa upande wa Mradi wa Mkuranga, Luhemeja alisema unatekelezwa na Dawasa. Baada ya Dawasa kukabidhiwa rasmi eneo hilo la Mkuranga hivi karibuni, imeanza kulaza mabomba ya usambazaji maji kwa urefu wa kilometa 63.5 na ujenzi wa tangi kubwa la maji, lenye uwezo wa kuhifadhi maji ya ujazo wa lita 1,500,000. Mradi huo utanufaisha wakazi 25,500 wa wilaya hiyo, hasa wa maeneo ya Mkuranga A, Mkuranga B, Kiguza, Mgawa, Bigwa, Mkwalia, Kitumbo, Njia nne, Sunguvuni na Hoyoyo.

Kazi ya ulazaji mabomba ya usambazaji maji imefikia asilimia 97 na kazi ya ujenzi wa tangi kubwa la maji imefikia hatua nzuri.

Chanzo: habarileo.co.tz