Wadau wa kupinga ukatili mkoani Mwanza wametaja tatizo la kisaikolojia kwa wanaume kuwa chanzo cha kuonekana wao ni wahusika wakuu wa vitendo hivyo katika jamii.
Wakizungmza Julai 9, 2023 kwenye kikao cha Mashujaa wa Kupinga Ukatili Mkoa wa Mwanza (Smaujata) wametaja sababu zingine za vitendo hivyo kwa wanaume ni ulevi na madawa ya kulevya, malezi, mila na desturi, ukosefu wa elimu kuhusu ndoa, imani, hisia na uhalisia.
Mjumbe Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Pamba mkoani Mwanza, Hamza Magesa amesema matukio ya ukatili yanazidi kutokea katika jamii kutokana na tatizo la afya ya akili ambalo limekuwa likiwakumba wanaume wengi nchini kutokana na umaskini na ukosefu wa elimu.
“Katika nchi yetu tuna tatizo la afya ya akili lakini pia imegundulika kuwa vijana wengi wa kiume wamekuwa wakijihusisha na ulevi na uvutaji bangi, tuna uhakika pia ongezeko la pombe linasababisha ongezeko la afya ya akili sasa kwa sababu wanaume ndo mashujaa wa hayo mambo ndio maana unaona wanakuwa wahanga,”amesema Magesa
Teddy Chande, kutoka Kambi ya Twende Kitalii ametaja imani potofu, hisia na malezi katika jamii zimekuwa na mchango mkubwa kwa wanaume wengi kujiingiza katika matukio ya ukatili.
“Katika hisia tunasema usifanye jambo ambalo unaweza kushindwa kulitolea maelezo kwa sababu ya hisia kwa sababu hisia zinaweza kukufanya ufanye maamuzi mazuri au mabaya sasa kwa upande wa mwanaume kuna muda anakuwa kama kichaa pale anaposhindwa kuzuia hasira ndio maana kuna wakati wanafanya mambo ambayo baadaye wanakuja kujutia,”amesema Chande
Mwenyekiti wa Hamasa Smaujata Mkoa wa Mwanza, Jumanne Bariana ametoa wito jamii kuachana na imani potofu zinazochochea vitendo vya ukatili, badala yake wajikite kutafuta njia nzuri za kuondokana na ukatili katika jamii ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya viashiria na vitendo hivyo.
“Mbinu za kizamani katika ndoa kwa miaka ya sasa ni ukatili mfano kipindi cha nyuma mwanaume alikuwa akimpiga mke wake akiwa na lengo la kumfundisha lakini kwa sasa mwanaume anampiga mke wake kwa kumkomoa na sio tena kumfundisha,”amesema
“Ni waombe wanaume kuachana na vitendo vya ukatili katika jamii lakini pia tunajua mmekuwa mkifanyiwa vitendo hivyo jitahidini kutoa taarifa katika vyombo husika ili kupata msaada na kuhakikisha tuna tokomeza kabisa vitendo hivi katika jamii,”amesema Bariana
Mtaalamu wa Saikolojia na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Iringa Kitivo cha Saikolojia, Robert Lwiza ametoa wito kwa jamii kuachana na dhana ya kuamini watendaji wakuu wa ukatili ni wanaume badala yake waamini mtu yoyote bila kujali jinsia anaweza kuwa na tatizo la afya ya akili na kufanya kitendo hicho.
“Tatizo la afya ya akili ni tatizo la kila mtu sio kweli kwamba wanaume ni wahusika wakuu wa ukatili, wanawake hawaonekani zaidi kwa sababu wao wanachukuliwa kama kundi la wanyonge lakini na wao wanafanya kwahiyo katika kupima hili tunatakiwa kuangalia namna unavyofanyika,”
“Katika kutatua tatizo hilo tunachotakiwa kukifanya ni kutafuta njia nzuri ya kuwatatulia matatizo ya afya ya akili kwa watu wote bila kuangalia jinsia,”amesema Lwiza