Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Wizara wa Fedha na Mipango imekamilisha tathmini ya watu waliopisha ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).
Majaliwa ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa nyumba 1,000 zinazojengwa mkoani Dodoma na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Majaliwa amesema wizara hiyo inaandaa malipo kwa ajili ya watu hao na yatatolewa hivi karibuni.
Amesema pia mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru anaandaa hati kwa wananchi waolikuwa jirani na SGR ambao maeneo yao hayajachukuliwa.
Amesema watu hao hawakupata hati kwa sababu walikuwa wakisubiri SGR wachukue eneo walilokuwa wakihitaji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umeme.
Awali mbunge wa Dodoma, Anthony Mavunde alimuomba Waziri Mkuu kutilia msukumo Hazina na Shirika la Reli Nchini (TRC) kuwalipa wakazi hao ambao wamekubali kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi.
Akizungumzia kuhusu mradi huo, mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dk Maulidi Banyani amesema awamu ya kwanza ya mradi wa nyumba 1,000 ulianza Januari 6, 2021 kwa Iyumbu na Chamwino ulianza Februari 1, 2021.
Amesema mradi huo unaohusisha ujenzi wa nyumba za makazi 1,000 mkoani hapa utagharimu Sh71 bilioni hadi kukamilika.
“Awamu hii ya kwanza yenye nyumba 404 itagharimu Sh21.4 bilioni na kazi kubwa ya ujenzi itakuwa imekamilika ifikapo Desemba 2021 na kubakiwa na ukamilishaji wa kazi chache za nje ambazo nazo zitaisha mwezi Januari 2022,”amesema.