Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tarura yalia na halmashauri Meatu,Bariadi

2533a92df4884f031ceb13996e0cbb59.png Tarura yalia na halmashauri Meatu,Bariadi

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKALA wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Simiyu unadai Halmashauri za Wilaya za Meatu na Bariadi Vijijini zaidi ya Sh milioni 134.

Kutokana na deni hilo, umeomba uongozi wa mkoa huo kusaidia kupata fedha zake hizo.

Ombi hilo lilitolewa jana na Mratibu wa Wakala huo Mkoa, Dk Philemon Msomba wakati wa kikao cha bodi ya barabara mkoa, ambapo alisema wanazidai halmashauri hizo zaidi ya Sh milioni 134.

Msomba alisema kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Tarura inadai zaidi ya Sh milioni 97.5 na Bariadi Vijijini wanadai zaidi ya Sh milioni 37.1. Alisema wanadai fedha hizo tangu mwaka 2017.

"Halmashauri hizi zilitumia fedha hizi kutoka Mfuko wa Barabara, baada ya Tarura kuanzishwa tulikuta tayari wamezitumia. Tukaendelea kuwadai lakini mpaka leo hawajazirejesha. Tunaomba viongozi wa mkoa, mtusaidie tupate fedha hizi ili tuwalipe wanaotudai," alisema Msomba.

Katika kikao hicho, mratibu huyo alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2020/21, Tarura imepanga kutumia Sh bilioni 5.1 kwa ajili ya ukarabati wa madaraja na barabara kilometa 822.

Aliwaomba wabunge wa mkoa huo, kuipigania Tarura ili iweze kuongezewa mgawo wa fedha kutoka Mfuko wa Barabara, kwani kwa sasa wanapatiwa asilimia 30 huku Tanroads wakipata asilimia 70.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa (Tanrods), Albert Kent akiwasilisha makisio ya bajeti ya mwaka 2020/21, alisema wamepanga kutumia Sh bilioni 11.4 kwa ajili ya matengenezo ya kilometa 900 za barabara na madaraja.

Kwa upande wao, wajumbe wa kikao hicho wakiwemo wabunge, waliiomba serikali kuiongezea bajeti Tarura, kwani kiasi cha fedha ambacho wanapewa kwa sasa ni kidogo kulinganisha na mtandao mkubwa wa barabara.

Chanzo: habarileo.co.tz