Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tarura wapongeza viwango uboreshaji Dar

8765c8a14588b81df63c0c74489f7c05 Tarura wapongeza viwango uboreshaji Dar

Fri, 9 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BODI ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) imepongeza ubora wa viwango wa miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya mpango wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam(DMDP).

Akizungumza wakati wa ziara ya kuitembelea miradi hiyo ikiwemo ya barabara, hospitali, masoko pamoja na mifereji katika wilaya ya Temeke, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Floria Kabaka, alisema umefika wakati kwa wananchi kujivunia miradi hiyo kutokana na ubora wake na kuitunza ili iwanufahishe.

Alisema miradi hiyo iliyojengwa kwa fedha nyingi, inatoa nafasi kwa wananchi waliopo katika eneo lenye mradi kufanya shughuli za kujenga uchumi pasipo changamoto zozote hususani upande wa masoko na barabara mbalimbali ambazo hapo awali zilikuwa vikwazo kwa watumiaji wengi.

“Miradi hii imejengwa kwa fedha nyingi ambazo zingeweza kufanya shughuli zingine, kwetu kama watekelezaji wake hatutofurahia kuona baadhi ya watu wakiitumia vibaya,” alisema.

Alisema miradi hiyo hususani mifereji kwa kiwango kikubwa imeweza kuokoa baadhi ya makazi ya watu ambayo hapo awali yalikuwa katika hatari kutoweka kwa kusombwa maji hivyo wananchi hawana budi kuitunza ili iweze kuwasaidia.

Aidha kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tarura, Victor Sefu, alisema licha ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika miradi hiyo, faida itokanayo na uwepo wake ni kubwa na yenye manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Alisema walichokibaini katika miradi mingi hususani ya barabara na mifereji ni uwepo wa taka nyingi zinazosababisha mifereji hiyo kuziba, kwamba jukumu walilonalo kwa sasa ni kuhakikisha wanaifanyia kazi kwa lengo la kuondoa adha hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz