Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tarime wahakikishiwa mbegu bora za mahindi

7a32096b9ecefa313c9b127443489925 Tarime wahakikishiwa mbegu bora za mahindi

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo imesema itahakikisha wakulima wa Wilaya ya Tarime na mMkoa wote wa Mara wanapata mbegu bora za mahindi na mbolea kwa bei elekezi ya serikali ili kudhibiti biashara ya magendo mpakani.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya juzi alipozungumza na wakulima wa Kijiji cha Nyamwaga wilaya ya Tarime wakati alipokagua mashamba darasa ya kahawa, mihogo na migomba.

Kusaya alisema kutokana na malalamiko ya wakulima wa Tarime kusema hawapati mbegu bora za mahindi na mbolea zinazozalishwa nchini hali inayowafanya wategemee bidhaa hizo toka Kenya zinazoingizwa kinyemelea mpakani Sirari.

Akizungumzia suala la uhaba wa mbegu na mbolea, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mtemi Msafiri alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa wakulima wanapata shida ya kupata pembejeo za serikali na kuwa Tarime hazifiki hali inayowafanya wakulima kushindwa kuzalisha kwa tija mazao hususani mahindi yanayotegemewa kwa chakula.

“Tuna shida kubwa ya mbegu bora za mahindi hapa Tarime na zinazopatikana zinauzwa bei kubwa mfano kilo mbili kwa Sh 15,000 na nyingi zinatoka nje ya nchi,”alisema.

Kusaya aliwahakikishia wakulima hao kuwa wizara yake kupitia Wakala wa Mbegu (ASA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) utafikisha mbegu za mahindi, alizeti na mbolea mkoani humo mapema kabla ya Desemba mwaka huu .

“Nimeagiza Mtendaji Mkuu wa ASA, Dk Sophia Kashenge afike hapa Mara na ahakikishe mbegu bora za mahindi zinauzwa kwa bei elekezi ya serikali ili wakulima wengi wamudu na kutoendelea kuumizwa na wafanyabiashara. Mbegu hizi zitauzwa chini ya Sh 10,000,”alisema.

Akiwa kijijini Nyamwaga kwenye mkutano wa hadhara wakulima walieleza kuwa wanauziwa mbolea aina ya NPK mfuko wa kilo 50 kwa bei ya Sh 60,000 hadi 80,000 kwa inayotoka Kenya na ya Tanzania kwa Sh 80,000 hadi 100,000 hivyo kushindwa kumudu.

Katika hatua nyingine Kusaya aliwashauri wakulima wa wilaya ya Tarime pamoja na kulima mazao ya chakula wajikite pia kuzalisha mazao ya kahawa, chai na migomba yanayostawi vema kutokana na hali ya hewa nzuri na kuwa wizara yake itatoa utaalamu na pembejeo ikiwemo mbegu bora.

Kusaya aliongeza kuwahakikishia wakulima wa migomba na mihogo kuwa tatizo la wadudu wasumbufu litapatiwa suluhisho mapema kupitia taasisi ya Utafiti wa kilimo (TARI) ambapo watafiti watafika Tarime na Butiama kukutana na maofisa ugani na wakulima.

“Niwatoe hofu wakulima wa mihogo na migomba kuhusu tatizo la ugonjwa unaoharibu mazao hayo, kuwa wiki ijayo wataalamu toka TARI Maruku (Bukoba) na wale wa TARI Ukirigulu (Mwanza) watafika hapa Tarime kutatua changamoto za magonjwa haya kwa kuwafundisha maafisa ugani namna ya kukabiliana na wadudu hawa,”aliahidi.

Chanzo: habarileo.co.tz