Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tari Makutopora kutoa mafunzo ya kilimo

5165327af41857ff6aeb0aa1bff3e30e.png Tari Makutopora kutoa mafunzo ya kilimo

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) kituo cha Makutupora imejipanga kuanzisha kituo cha usambazaji wa teknolojia na taarifa za kilimo katika viwanja vya Maonesho ya Wakulima (Nanenane) Nzuguni mkoani Dodoma.

Kituo hicho kitatumika kutoa elimu kwa wakulima kwa kipindi cha mwaka mzima.

Akizungumza na HabariLEO ofisini kwake jijini hapa jana, Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk Cornel Massawe alisena hatua hiyo imetokana na mahitaji ya elimu ya kilimo hasa katika uandaaji wa mashamba na matumizi ya mbegu bora kwa wadau wa kilimo katika nyanda kame kuongezeka.

Alisema taasisi hiyo imeona muda wanaoupata wakulima kipindi cha sherehe za Nanenane ni mfupi ikilinganisha na mahitaji ya wadau hao ambao wanahitaji taarifa na elimu ya kutosha kwa kipindi cha mwaka mzima.

Dk Massawe alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuhakikisha teknolojia na taarifa zinawafikia wadau wote wa kilimo katika nyanda kame ambazo ni mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora na kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Alisema kituo hicho kitakuwa na aina 17 za mazao, zabibu, mtama, ulezi, uwele, kunde, alizeti, mbaazi, karanga, ufuta, mahindi, mihogo, viazi, korosho, migomba na choroko.

“Kituo hiki kinalenga kuazisha bustani ya mipapai, pia kuna aina ya mtama wa malisho mbao hutumika kama malisho ya mifugo baada ya mkulima kuvuna mtama wake.”

“Mkulima atafika kwa muda wake kwa ajili ya kujionea na kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo kwa lengo la kuboresha kilimo chake ili kupata tija,” alisema.

Dk Massawe alisema wanategemea kupata wadau wa kilimo kutoka katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kujifunza katika kituo hicho.

Aidha, alisema kuanzia Agosti hadi Desemba, mwaka jana wakulima 61 kutoka maeneo ya wilaya za Chamwino, Bahi na Dodoma Jiji walijifunza aina mbalimbali za zabibu, namna ya kuhudumia mizabibu na namna ya kutengeneza mvinyo pamoja na kuomba mbegu bora za zao hilo.

Alisema pia wakulima 25 kutoka mikoa Tabora, Dodoma na Singida walifika katika vitalu vya zao la korosho ili kujifunza namna ya uzalishaji, pamoja na mahitaji yake, mbolea na namna ya kudhibiti wadudu.

Alisema wakulima 75 kutoka mikoa ya Morogoro na Dodoma nao walifika kwa ajili ya kujifunza kuhusu zao la mahindi na wakulima 240 walifika kujifunza kuhusu zao la muhogo.

Mratibu wa utafiti na ubunifu wa kituo hicho, ambaye pia ni mratibu wa kitaifa wa zao la zabibu, Saada Hussein alisema kitasaidia wakulima kujifunza aina zote za mazao kwa muda wa mwaka mzima.

Chanzo: habarileo.co.tz