Msimamizi mkuu wa matengenezo ya barabara na madaraja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Mororgoro, Mhandisi Patrick Rambika amesema Serikali imesaini mradi wa ujenzi wa barabara ya Ubena Zomozi hadi Ngerengere (Kizuka Army Camp) tayari kuanza ujenzi.
Mradi huo wenye urefu wa kilomita 11.6, umesainiwa leo Alhamisi, Februari 7, 2024, kati ya Serikali na mkandarasi mzawa, M/s Kings Builders Ltd atakayetekeleza mradi huo kwa gharama ya Sh20.54 bilioni kwa muda wa miezi 12.
Aidha, mradi mwingine wa ujenzi wa barabara ya Bigwa hadi Kisaki sehemu ya Bigwa hadi Mvuha, wenye kilomita 78, mkataba umesainiwa Februari 5, 2024 na Mkandarasi M/s China Railways 15 Bureau Group Corporation ya China utakaotekelezwa kwa gharama ya Sh132 bilioni kwa muda wa miezi 27.
Rambika ameeleza hayo leo Alhamisi, Machi 7, 2024 alipozungumza na kipindi cha Tanroads mkoa kuhusu mafanikio ya Serikali katika sekta ya miundiombinu ya ujenzi wa barabara na madaraja.
"Mradi wa ujenzi wa barabara ya Ifakara kwenda Kihansi, Mlimba, Taweta hadi Madeke Sehemu ya Ifakara hadi Mbingu wenye kilomita 62.5 na mkataba ulishasainiwa, mkandarasi ameshakabidhiwa na ameanza kazi ya kujenga kambi na kuleta mitambo ya ujenzi.
“Pia, Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kitaifa mkoani Morogoro ikiwemo ujenzi wa barabara ya Mikumi hadi Kidatu mpaka Ifakara (sehemu ya Kidatu – Ifakara, (km 66.9) kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa daraja la Ruaha Mkuu ambao umefikia asilimia 86 za utekelezaji na tayari mkandarasi amekamilisha kilomita 55.67 za lami kati ya kilomita 66.9 zinazotakiwa kwa mujibu wa mkataba,” amebainisha.
Aidha, amesema ujenzi wa barabara ya Dumila, Kilosa hadi Mikumi (kilomita 142) utafanyika kwa kwa kiwango cha lami (sehemu ya Rudewa Kilosa km 24) kwa kutumia fedha za ndani.
“Mkandarasi amekamilisha ujenzi wa kilometa 22.05 barabara imekabidhiwa na inatumika, amekamilisha pia madaraja matatu ya Kobe, Wailonga na Mazinyungu na kwa sasa anaendelea na kazi ya kilomita 0.75 ya maungio ya madaraja hayo,” ameeleza.