Wilaya ya Tanganyika imekamilisha ujenzi wa vyumba 196 vya madarasa huku zaidi ya Sh100 milioni zikibaki katika utekelezaji wa mradi huo iliyojengwa kwa fedha za Uviko-19.
Akisoma taarifa kwa Mkuu wa mkoa kwenye makabidhiano yaliyofanyika shule ya sekondari Kabungu, ofisa Mipango wa wilaya hiyo, Dotto Kwigema amesema walipokea Sh5.4 bilioni kwa ajili ya mradi huo.
Amesema Serikali ilielekeza Sh1.38 bilioni kutekeleza ujenzi wa vyumba 69 vya madarasa katika shule za sekondari na kwamba vimekamilika na kugharimu Sh1.4 bilioni.
“Sh34 milioni zimebaki shule za msingi tulielekezwa kutumia Sh2.5 bilioni kujenga madarasa 127 tumekamilisha, fedha zilizotumika ni Sh2.4 na Sh.84 milioni zimebaki,” amesema Kwigema
“Fedha zilizobaki zitatumika kujenga matundu 144 ya vyoo katika shule za msingi na matumizi mengine,”
Mkuu wa Wilaya hiyo, Onesmo Buswelu amesema jografia ya wilaya hiyo siyo rafiki lakini walifanya jitihada za kuyafikia maeneo yote kuhakikisha ujenzi unakamilika.
Advertisement
“Tumefanya kazi usiku na mchana, tunawashukru sana wananchi shule za msingi wamechangia Sh107 milioni, sekondari Sh38 milioni,” amesema Buswelu.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko baada ya kukabidhiwa madarasa hayo amesema asilimia kubwa ya madarasa yaliyojengwa kwa fedha za Uviko-19 yapo wilaya ya Tanganyika.
“Mngeanguka Tanganyika ungeanguka mkoa mzima kwasababu mlibeba zaidi ya asilimia 46 ya madarasa yote, hongereeni sana, fedha mmebakiza,” amesema Mrindoko akaongeza.
“Andikeni mapendekezo yenu fedha zilizosalia zitumike kwenye miradi gani ya elimu, leteni ofisini kwangu nitakaa na kamati yangu tushauriane, tutoe maelekezo ya matumizi,”