Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanga ya pili usafirishaji, uingizaji dawa za kulevya Tanzania

Drugs Dawa za Kulevya

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, mkoa huo, siyo kwamba tu ni kituo cha usambazaji, bali pia una idadi kubwa ya watumiaji wa dawa hizo.

Akizungumza jana, wakati akizindua mradi wa ‘The Bright Future’ unaolenga kuimarisha usafi wa mazingira katika Jiji la Tanga, alisema kutokana na hali hiyo kushamiri, ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kutafuta namna bora ya kudhibiti mianya ya uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya.

“Kwa kweli niwapongeze sana watu wa Gift of Hope, kazi mnayofanya ni kubwa mno, kwa namna mnavyopambana kushinda matumizi ya dawa za kulevya. Kazi hii inataka moyo sana, na mradi huu ni maamuzi mazuri ya kuona mnashiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali,” alisema na kuongeza:

“Lakini natoa rai kwa vijana ambao wamefanikiwa kuondoka katika uraibu wa dawa za kulevya, kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili wawe mfano kwa mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa watu wengine walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Malima.

Mradi huo wa The Bright Future, unalenga zaidi kukusanya taka ngumu za plastiki na kutumia dhana ya urejeshaji wa taka hizo katika hali ya ubora na thamani.

Aidha, Malima alisema kimsingi mradi huo licha tu ya kuimarisha usafi wa mazingira, pia ni chanzo kikuu cha mapato kwa vijana watakaoshiriki shughuli hizo.

Awali, Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Zamoyoni Mohamed, akizungumza kabla ya uzinduzi wa mradi huo, alisema watatoa ushirikiano mkubwa kwa wadau hao ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Watu wa Tanga, tupo katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ambao taka za plastiki zisipodhibitiwa vizuri, zinaleta madhara hata kwa viumbe hai wa baharini,” alisema Mohamed.

Zamoyoni alisema kuwa halmashauri itashiriki katika kuhakikisha taka hizo za plastiki zinafikishwa kwenye maeneo yanayopaswa, hasa kwenye viwanda ambavyo hutumia malighafi hizo kuziongezea thamani ikiwamo kutengeneza mikeka na matofali.

Katibu Mtendaji wa Asasi ya Gift of Hope, Said Bandawe, alisema mradi huo wa The Bright Future, unajihusisha na ukusanyaji wa chupa za plastiki zinazotupwa kwenye maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ya watu.

Bandawe, alisema mradi unajumuisha waraibu 20, ambao watahusika katika usimamizi na utekelezaji wa kukusanya chupa chakavu za plastiki na ngumu.

Kwa mujibu wa Bandawe ni kwamba mradi umelenga kuwafikia vijana 200 kwa awamu ya kwanza na kuihamasisha jamii kuachana na tabia hatarishi kwa kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali na kuondokana na utegemezi.

Chanzo: ippmedia.com