Halmashauri ya Jiji la Tanga imekuwa ya pili kufanya mabadiliko ya kiutendaji kutoka kwenye mfumo wa zamani na kuhamia katika matumizi ya mfumo wa kisasa kwa kununua vishikwambi 64 kwa ajili ya madiwani, wakuu wa idara, vitengo vya halmashauri hiyo.
Akikabidhi vitendea kazi hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema amesema kuwa lengo la kuhamia katika mfumo wa digitali ni kuokoa gharama, ambazo zimekuwa zikitumika kwa ajili ya uendeshaji wa vikao ndani ya halmashauri.
“Kwa kuingia kidigitali sasa hamna umuhimu sana wa kuingia gharama ya kuchapisha karatasi, kwani matumizi ya teknolojia ya vishikwambi itamaliza tatizo hilo,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Dk. Sipora Liana, amesema kuwa vitendea kazi hivyo vitaboresha utawala bora na kwamba itakuwa halmashauri ya pili kwa manunuzi na ugawaji wa vishikwambi nchini baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Vishikwambi hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 101 vimegharamiwa na halmashauri ya jiji hilo.