Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanga walivyorahisishiwa kupata vyeti vya kuzaliwa

44a01dfb631303d4edcf8ec5b739af95.png Tanga walivyorahisishiwa kupata vyeti vya kuzaliwa

Mon, 10 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KULTHUM Juma, mkazi wa Tanga mjini, anasema kichwa kilikuwa kinamuuma kila akifikiria atakavyomwandikisha mwanae shule kwani moja ya sharti ni kuwa na cheti cha kuzaliwa.

Anasema hata chekechea alikompeleka walikuwa wakidai cheti hicho ingawa walimpokea huku yeye akiahidi kukishughulikia.

‘Mtihani’ huo ndiyo aliyokuwa nao Zuwena Kipara, mkazi mwingine wa Tanga ambaye alikuwa ameshindwa kuanza kumwandikisha mwanae mdogo ili kupata bima kupitia ofisini kwa mumewe anayefanya kazi serikalini kutokana na mwanae huyo kukosa cheti cha kuzaliwa ambacho ni sharti muhimu.

“Yaani mwanangu akiumwa nalazimika kumtibu kwa akiba yetu ya ndani wakati angeweza kutibiwa kwa bima. Lakini nilipoteza tangazo la hospitali na hivyo nikawa sijui nianzie wapi katika kumtafutia cheti cha kuzaliwa,” anasema.

Lakini wazazi hao wawili na wengine sasa wana furaha tele baada ya kupata vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wao kwa urahisi sana tofauti na walivyotarajia.

Hii ni kutokana na hatua ya Mkoa wa Tanga, kama ilivyo kwa Mkoa wa Kilimanjaro kuja na mpango wa usajili wa vizazi na utoaji vyeti kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Mpango huo ambapo ulizinduliwa na mwezi Agosti mwaka jana na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo, Dk Mwigulu Nchemba, ulilenga kusajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto bila ya malipo.

Madhumuni mengine ya hatua hiyo ni sambamba na kuongeza kiwango cha usajili na kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anapatiwa cheti kwa wakati.

Vile vile mpango huo ulilenga katika kugatua madaraka kwa kusogeza huduma za usajili karibu na wananchi, yaani kwenye hospitali pamoja na ofisi za kata sambamba na matumizi ya Teknolojia ya Mawasiliano (Tehama) katika usajili ili kuinguza kwenye kanzi data .

Hivi karibu mkoa wa Tanga ulifanya kikao cha tathimini ya mpango huo kilichojumuisha wadau kutoka Wakala wa Usajili Ufilisi na

Udhamini (RITA), wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji na viongozi wengine ngazi ya mkoa na wilaya.

Tathmini ililenga kuwashirikisha wadau hao kuhusu hali na maendeleo ya utekelezaji wake, mafanikio, changamoto na kushauri maboresho gani yafanyike ili kuhakikisha watoto wote wanasajiliwa ili kuepuka kutengeneza bakaa.

Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa Rita, Emmy Hudson, anasema kuwa mpango huo ambao unafadhiliwa na serikali ya Tanzania pamoja na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kupitia idara ya mambo ya nje, biashara na maendeleo.

Anasema kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo kumeleta maboresho makubwa katika usajili wa vizazi na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto ikiwemo kusogeza huduma karibu na maeneo ya makazi ya wananchi.

Anasema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa imetatua changamoto iliyokuwa ikiwakabili wananchi ya kutumia gharama kubwa na muda mwingi wa kufuata huduma hizo katika ofisi za wakuu wa wilaya, hali ambayo ilisababisha idadi ndogo ya watoto waliosajiliwa.

Kaimu Kabidhi anaema tathimini inaonyesha katika kipindi cha mwaka mmoja ya utekelezaji wake, mkoa umeweza kuongeza kiwango cha usajili kutoka asilimia 9.9 tu yawatoto watoto waliokuwa wamesajiliwa hapo awali hadi kufikia asilimia 80.1, sawa na watoto 291,962 ya waliotarajiwa kusajiliwa.

“Haya ni mafanikio makubwa sana kwa mkoa na Taifa kwani Rita tunaamini mafanikio haya yanatokana na nia ya dhati iliyoonyeshwa na viongozi wa mkoa toka hatua za awali za utekelezaji wa mpango huu,” amesema Hudson

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella, ambaye alikuwa ni mgeni rasmi katika kikao hicho amewataka wakuu wa wilaya zote za mkoani hapa kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu na kuhamasisha wananchi kusajili watoto wao chini ya umri wa miaka mitano ili waweze kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.

Anasema kuwa licha mpango huo kufanya vizuri, takwimu zinaonyesha kuwa Wilaya ya Mkinga inaonekana kuwa na asilimia ndogo ya watoto waliosajiliwa ya asilimia 34 pekee wakati wilaya nyingine zimefikia zaidi ya asilimia 50.

“Sio kwamba kazi katika wilaya hii haikufanyika bali ilibidi kuwe na mfumo tofauti wa usajili kutokana na eneo hilo kuwa na mwingiliano mkubwa na wananchi wa nchi jirani ya Kenya hivyo kusababisha walengwa kushindwa kufikiwa,” anasema Shigella.

Shigella anawataka wakuu wa wilaya kushirikiana na Waganga wakuu wa wilaya kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa katika hospitali na vituo vya afya wanapata usajili kwani bado kuna watoto wengi mitaani wasio na vyeti hivyo ipo haja ya kuendelea kuhamasisha zoezi hilo ili kuleta mafanikio makubwa zaidi.

“Mafanikio tuliyoapata yanatakiwa kudumishwa na kuwa endelevu kwani tusipokuwa makini tutajikita tunarudi chini katika zoezi hili. Nataka tuongeze juhudi ili ifikapo mwishoni mwa mwaka huu tuweze kusajili watoto kwa asilimia 100,” anasema Shigella.

Hata hivyo, Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu anasema tathmini ndogo iliyofanywa katika kanzidata ya Rita inaonyesha kuwa katika mkoa wa Tanga vipo vituo ambavyo havijaingiza taarifa kwa kipindi cha miezi kadhaa kuonesha kwamba aidha havijasajili au vinasajili lakini haviingizi taarifa na kutuma kwenye kanzidata.

“Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu tumeweza kusajili watoto1,403 sawa na asilimia tu wakati lengo ilikuwa ni kusajili zaidi ya asilimia 22, hivyo ipo haja ya kuhakikisha tunaongeza kasi ya uhamasishaji kwa jamii kuona umuhimu wa watoto wao kuwa na vyeti vya kuzaliwa,” anasema Hudson.

Anasema mpango huo wa usajili na utoaji wa vyeti ni endelevu na sio wa muda mfupi na kwamba vituo vinavyotoa huduma ni vyakudumu na vitaendelea kutoa huduma hiyo bila ya kikomo.

“Napenda kutoa rai kwa viongozi wenzangu tuendelee kusimamia na kuhakikisha huduma hii inaendelea kutolewa kwa kila mwananchi anayestahili katika maeneo yao,” anasisitiza Hudson.

Katika kikao hicho cha tathmini, watendaji wanaziomba halimashauri kuweka mikakati endelevu ya kuhamasisha zoezi hilo ili liweze kuwa endelevu badala ya kuonekana ni la kipindi maluumu tu.

Mkurugenzi wa Halimashauri ya Wilaya ya Handeni, Willium Makufwe anasema kuwa waliweka lengo la kusajili watoto 10,952 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu badala yake wamesajili watoto 148 tu sawa na asilimia 1.4%.

“Ningewaomba viongozi wa kisiasa kama madiwani kuendelea kufanya uhamasishaji katika maeneo yenu ili wazazi na walezi waone umuhimu wa kusajili watoto wao na kupatiwa cheti bure wakiwa katika hatua za awali za makuzi yao,” anasema mkurugenzi huyo.

Nae Mwenyekiti wa Halimashauri ya wilaya ya Korogwe, Sadik Kallaghe anazitaka halimashauri kuweka mikakati ya kuandikisha kila mtoto ambaye anazaliwa kwa wakati na taarifa zao kutumwa Rita ili hatua zinazofanyika zionekane.

“Sisi halimashauri ndio wenye vituo vya afya ambavyo tunashukuru namna ambavyo serikali imeweza kuviboresha na vingi vina huduma ya mama na mtoto, sasa hapo tuna sababu gani ya kushindwa kupata watoto ambao hawajasajiliwa?“ Anahoji Kalaghe.

Chanzo: www.habarileo.co.tz