Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanga wajipanga kutumia fursa za bomba la mafuta

Ad017ca30a12f2e3b5803c3c9d782dc7 Tanga wajipanga kutumia fursa za bomba la mafuta

Tue, 22 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela Alhamisi wiki hii anatarajiwa kukutana na wadau watakaoshiriki katika mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP), litakaloishia eneo la Chongoleani mkoani humo.

“Siku ya Alhamisi wiki hii nitafanya kikao na wadau wa bomba la mafuta kuwaeleza taarifa ya serikali kuhusu mradi huu wa ujenzi wa bomba la mafuta, hadi ninyi watu wa vyombo vya habari mtaalikwa,”alisema Shigela kwa njia ya simu.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa alisema serikali wilayani humo imejiandaa katika maeneo yote kuanzia ulinzi na usalama, usaidizi na masuala ya kiuongozi kuhakikisha mradi unatekelezwa kama ilivyopangwa.

Alisema wananchi ambao wana mali katika maeneo ambayo ramani inaonesha kuwa bomba lenye urefu wa kilometa 1,445 litapita, wamekubali kuyatoa na kulipwa fidia kupisha ujenzi huo.

“Wilayani kwangu maeneo yote ambapo ramani inaonesha kuwa bomba litapita wananchi wamekubali kuyatoa kwa kiasi hicho cha fidia, ambacho serikali imepanga kulingana na thamani ya mali zao.

Mwanzoni walikuwa wanalalamika na mfano ni wakazi wa Kijiji cha Chongoleani ambapo kutajengwa matenki makubwa ya kuhifadhia mafuta, wamekuja na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tanga (CUF) Mussa Mbarouk baada ya kuwaelimisha wameelewa,”alisema Mwilapwa.

Alisema Ijumaa iliyopita alimalizia kusaini majedwali makubwa manne, yanayoonesha namna wananchi wilayani humo wakakavyofidiwa na kiasi cha fedha.

“Na kila mtu ameridhika, pia nimekutana na kamati yangu ya ulinzi na usalama ya wilaya kuhusu hali ya usalama Chongoleani (bomba litakapoishia), kuko shwari, hata miundombinu iliyowekwa awali wakati wa uzinduzi wa bomba hilo haijaharibiwa”alisema Mwilapwa.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni,Toba Nguvila alisema wananchi wa wilaya hiyo, wamepokea kwa furaha taarifa ya Rais John Magufuli na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kukubaliana kuanza utekelezaji mradi huo.

Alisema, ofisini yake imepokea barua kutoka EACOP kumfahamisha kuwa Oktoba 2 mwaka huu, watakwenda kusaini majedwali kwa ajili ya wananchi kulipwa fidia.

Nguvila alisema wananchi wa eneo la Misima, ambako sehemu kubwa ya bomba hilo litapita, wamekubali maagizo ya serikali ya kulitoa eneo hilo na mali zao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa mradi huo.

Alisema, wananchi wamekubali hayo, baada ya serikali kwa kushirikiana na EACOP kutoa elimu kuhusu umuhimu wa mradi huo kwa uchumi wa nchi na kwao.

“Nataka nikuhakikishie kuwa wananchi wa Handeni wamepokea kwa furaha ujio wa bomba hili na wamekubaliana na maagizo ya serikali kutoa maeneo yao na mali zao kwa ajili ya kuanza ujenzi huo, na hivi ninavyoongea na wewe tayari barua ya watu wa bomba la mafuta ipo mezani kwangu kwa ajili ya kutia saini majedwali kwa ajili ya wananchi kulipwa fidia,”alisema.

Kuhusu fursa za ajira na uchumi, Nguvila alisema amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kupitia upya asilimia 10 ya mikopo ya makundi maalumu ili kuwakopesha akinamama, kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kutoa huduma za vyakula kwa wafanyakazi watakaofanya kazi kwenye eneo la mradi.

Alisema amewaagiza maofisa maendeleo ya jamii, kuwahamasisha akinamama kujiunga katika vikundi ili wakopesheke.

Nguvila alisema serikali wilayani humo imeendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu namna ya kuchangamkia fursa za ajira za moja kwa moja na za vibarua kwenye kampuni zitakazofanya kazi kwenye mradi huo.

Kuhusu malazi Nguvila alisema wilayani humo kuna hoteli za hadhi tofauti na kwamba wageni kutoka ndani na nje ya mkoa, watapata sehemu za kufikia au kuishi.

“Hapa Handeni ni moja ya sehemu ambazo kutajengwa ‘camp site’(kambi ya wafanyakazi) hivyo kutakuwa na watu wengi, kwa upande wa uwekezaji wa biashara ya kutoa huduma za vyakula na malazi hakuna wasiwasi”alisema Nguvila.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaasha Tumbo alisema wananchi wilayani humo wanafahamu na wapo tayari kuzitumia fursa, kwa kuwa wanaelewa nini kinaendelea.

Kuhusu huduma za kijamii katika eneo ambako kutajengwa kambi ya wafanyakazi, Tumbo alisema huduma zote muhimu tayari zipo.

Alisema, maji ya uhakika yameafikishwa hapo mwezi mmoja uliopita, kwenye eneo hilo kumejengwa Hospitali ya Wilaya ya Muheza na umeme ni wa uhakika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Brasian Makota alisema halmashauri hiyo wamejitahidi kuwahamasisha wananchi kutoa maeneo kupisha ujenzi wa bomba hilo.

Alisema mwanzo walikuwa wabishi, lakini sasa wameelewa na wapo tayari kwa hilo. “Tunatoa wito kwa wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa kampuni na wageni watakaokuja kwa ajili ya kuwekeza kwenye mradi huu na wahakikishe wanachangamkia fursa za ajira ndogondogo zitakazojitokeza,”alisema Makota na kuongeza;

“Sasa hivi tunashukuru wananchi wamekuwa waelewa, mwanzo kulikuwa na changamoto kubwa ya uelewa wa wananchi katika vijiji ambavyo bomba linapita, lakini baada ya kuwaelimisha na kuelewa umuhimu wake wamekubali na wapo tayari”.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Tanga, Rashidi Mwanyoka alisema baada ya Rais Magufuli na Rais Museveni kukubaliana kazi ianze, wameanza kuhamasisha wafanyabiashara kuanzia ngazi ya mama lishe, watoa huduma za hoteli na huduma nyingine kila mmoja kujipanga kushiriki katika mradi huo.

Alisema, mradi huo una wadau wengi kutoka serikali ya Tanzania, Uganda na kampuni kubwa kutoka ndani na nje ya Tanzania, hivyo wananchi hawana budi kujitokeza ili waweze kufaidika.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Tanga, Alfred Ndumbaro alisema barabara zote zitakazotumika kwa ajili ya mradi zinapitika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga WSSA), Geofrey Hilly alisema mradi wa kutoa maji Pongwe jijini Tanga kuyapeleka Muheza, katika sehemu ambayo kutajengwa kambi kubwa ya wafanyakazi, umekamilika na tayari yanafika.

“Mradi wa maji kutoka Pongwe kuelekea Muheza umekamilika kwa asilimia 100, tayari maji yanafika katika Kijiji cha Kitisa ambapo kuna tangi kubwa la kuyahifadhi kabla ya kuelekea Muheza mjini na hapo ndio kutajengwa kambi kubwa ya wafanyakazi, kwa hiyo huduma ya maji hakuna wasiwasi,”alisema Hilly.

Wananchi wa maeneo ya wilaya za Korogwe na Muheza na Kijiji cha Chongoleani wilayani Tanga, waliomba katika kila eneo mradi huo utakakopita, kusikosekane wanakijiji ambao watafanya kazi katika mradi ili nao wawe wanufaika.

“Hapa Chongoleani ndio eneo la Mamlaka ya Bandari (TPA) ambalo limetengwa kwa ajili ujenzi wa matangi ambayo mafuta ghafi yataishia hapa, sasa kwa sisi watu wa hapa ambao asilimia kubwa ni wavuvi, tunaiomba serikali vijana wetu waiingizwe katika shughuli za ujenzi na sisi wengine tupewe angalau zabuni ya kusambaza samaki”alisema Hamidu Juma, mkazi wa Kitongoji cha Putini, Chongoleani.

Joyce Shekizenghi, mkazi wa Kijiji cha Kwakombo Korogwe, aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe katika ujenzi wa bomba hilo, wawezeshe vikundi vya wanawake kwa kuwapatia mitaji ili kuanzisha biashara, ambazo na wao watatoa ajira kwa watu wengine ambao watawaletea bidhaa.

Mkoani Tanga bomba hilo linapita katika wilaya za Kilindi, Handeni, Korogwe, Muheza na Tanga na litaishia Kijiji cha Chongoleani, ambako kutajengwa matangi makubwa ya kuhifadhi mafuta ghafi. Agosti 5, 2017 Rais Magufuli na Rais Museveni waliweka jiwe la msingi eneo la Chongoleani mkoani Tanga.

Novemba 9 mwaka huohuo likawekwa jiwe la msingi eneo la Ruzinga Uganda. Septemba 13 mwaka huu mawaziri wa nishati wa Uganda na Tanzania, walisaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kugharimu shilingi trilioni 7.8.

Rais Magufuli na Rais Museveni walishuhudia tukio hilo kwenye Uwanja wa Ndege wa Chato mkoani Geita. Mkataba huo umesainiwa baada ya Rais Magufuli na Rais Museveni kukubaliana mgawanyo wa mapato.

Kwa kuzingatia makubaliano hayo, Tanzania itapata asilimia 60 ya mapato ya biashara hiyo ya mafuta na Uganda itapata asilimia 40.

Waziri wa Nishati, Dk Merdard Kalemani alisema katika kipindi chote cha miaka 25 na zaidi cha utekelezaji wa mradi huo, Tanzania itapata Sh trilioni 7.5.

Rais Magufuli alisema sehemu kubwa ya bomba hilo, ambayo ni kilometa 1,115 sawa na asilimia 80.1 ya urefu wa bomba lote, itapita Tanzania na zitakazobaki kilometa 330 zitapita Uganda.

Upande wa Tanzania mradi utapita mikoa minane, wilaya 24, kata 132, vijiji zaidi ya 186 na vitongoji 1,112. Magufuli aliitaja mikoa litakapopita bomba hilo kuwa ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Chanzo: habarileo.co.tz