Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanesco yawalipa fidia ya Sh2 bilioni wananchi 203

95392 Pic+fidia Tanesco yawalipa fidia ya Sh2 bilioni wananchi 203

Tue, 11 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Same. Wananchi 203 wa kijiji cha Kandoto Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro waliokuwa wakidai fidia baada ya mashamba yao kuchukuliwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wamelipwa Sh1.99 bilioni.

Malipo hayo yaliyofanyika leo Jumanne Februari 11, 2020 ni utekelezaji wa agizo la waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilolitoa Julai 2019 katika ziara yake wilayani Same baada ya kupokea malalamiko ya wananchi.

Eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 100 lilichukuliwa na Tanesco kwa ajili ya kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa kutumia jua ambao unatarajiwa kuzalisha Megawati 150 zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa.

Akizungumza wakati wa utoaji fidia hizo meneja wa Tanesco Mkoa wa Kilimanjaro, Mahawa Mkaka amesema eneo hilo lilikuwa ni mali za wananchi 301 waliopaswa kulipwa fidia ya Sh3.5 bilioni lakini wameanza awamu ya kwanza na wananchi 203 ambao wamelipwa Sh1.99 bilioni.

Wakizungumzia malipo hayo, Zenobia Msangi na Ayubu Abdalla mbali na kuishukuru Serikali kwa hatua iliyochukua na kuwezesha kulipwa fidia zao, wamesema fedha walizopewa watazitumia kuanzisha miradi ya maendeleo itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Tulianza kudai fidia mwaka 2016 tulifika mahali tukakata tamaa, tukidhani hatutalipwa lakini leo tumelipwa kila mtu haki yake aliyostahili, tunaishukuru sana Serikali, kwa hatua hii,” amesema Zenobia.

Pia Soma

Advertisement

Chanzo: mwananchi.co.tz