Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanapa yaombwa kuondoa tembo wasumbufu

13157 Pic+tembo Tanapa yaombwa kuondoa tembo wasumbufu

Mon, 15 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMLAKA ya Hifadhi ya Tanzania (Tanapa), imeombwa kuondoa tembo kwenye mashamba ya wananchi wa Kata Businde, wilayani Kyerwa, mkoani Kagera na kupelekwa wanapostahili.

Diwani wa Viti Maalumu wa kata hiyo, Consolata Kanyima, amesema tembo hao wanashambulia vijiji vya Businde na Bugela na kusababisha wananchi kuhama.

Alisema ni kipindi cha miaka mitano tangu Tanapa walipofika na kueleza watafanya uondoaji huo.

Vile vile, Kanyima alisema tembo huingia kwenye mashamba na kufanya ushambuliaji wa mazao.

"Wameshambulia maeneo hadi wananchi wamehama kwenda vitongoji vingine kuwapisha tembo, wameacha mashamba tunaomba watolewe watu warudi," alisema Kanyima.

Diwani wa Kata Songambele, Majaliwa John, alisema shughuli za wananchi zimekwama kutokana na eneo lililotegemewa kwa kilimo kuvamiwa.

John alisema, mwezi Machi wataalam wa Tanapa walitembelea eneo hilo na kuahidi kuondoa wanyama kwa kusaidia wananchi.

Kwa upande wake Kamshina wa hifadhi za Taifa pori la Ibanda, Kyerwa na Rumanyika, Murondo Murondo, alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo.

Murondo alisema, hatua iliyochukuliwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti Wanyama Pori (TAWIRI) walitembelea eneo hilo na kubaini idadi ya tembo kati ya 80 hadi 100.

Alisema, njia ya kuwaondoa ni kuwagawa kwa makundi matatu ambayo yatapita kwenye mashamba ya wanachi.

"Kama tunafahamu tembo ni mnyama wa porini na huwa hasahau njia yake ni tofauti na wanyama wa kufugwa kwamba watafukuzwa taratibu," alisema Murondo.

"Labda kuwaambia tu wananchi wasiwabugudhi hadi watakapopelekwa eneo la hifadhi ndiko sehemu sahihi," alisema Murondo.

Alisema Hifadhi ya Ibanda Kyerwa kuna vijiji 19 na Rumayika vipo 16 ambavyo vimezungukwa na hifadhi ya pori hilo.

Alisema mara nyingi wanyama pori huingia sehemu ambayo sio eneo lao na kufuata eneo ambalo limetulia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live