Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanapa kuweni makini corona watalii wanaoingia nchini

C2fbc64aed7fbd295469afd97354b804 Tanapa kuweni makini corona watalii wanaoingia nchini

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Rajab Kundya, amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 huku pia likiwahakikishia watalii kutoka mataifa mbalimbali kwamba Tanzania ni salama.

Alhaji Kundya aliyasema hayo wakati akiliaga kundi la watu 49 wakiwamo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanaopanda Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Tanganyika.

Miongoni mwa waliopanda ni mlima pamoja na wanahabari, wastaafu wa JWTZ, watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Tanapa.

Alisema pamoja na Tanzania kutokuwa na ugonjwa wa Covid-19ulioikumba dunia kwa jumla, bado ugonjwa huo upo hivyo, akaitaka Tanapa kuchukua tahadhari kwa watalii wanaokuja nchini ili kuhakikisha hakuna maambukizi yanayotokea.

Mkuu wa wilaya huyo kupitia ujumbe wa mwaka huu: "Mlima Kilimanjaro ni Salama, Panda Ukiwa Tanzania," alitaka Tanapa kutobweteka na tuzo za kimataifa zaidi ya tano ulizopata mlima huo, bali waendelee kuutunza ili uendelee kushika rekodi hiyo.

Alipongeza mpango madhubuti unaoandaliwa na JWTZ kila mwaka wa kupanda mlima huo kama sehemu ya maadhimisho ya miakaya Uhuru wa Tanganyika uliozaa Taifa huru la Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Alan Kijazi, Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa Kanda ya Kaskazini, Herman Batiho, alisema wataendelea kushikilia rekodi hiyo.

Alitaka wanaopanda mlima huo kuendelea kuutangaza nje ya mipaka ya Tanzania na kwamba, Tanapa itasimamia misingi ya kutunza vivutio vilivyopo nchini.

Katika zoezi la upandaji Mlima Kilimanjaro kwa kundi hilo la Watu 49, Mkuu wa Wilaya alikabidhi Bendera kwa kiongozi wa Askari wa JWTZ Kanali Msumari apandishe Bendera hiyo Mlima Kilimanjaro kama alivyofanya Alexander Nyirenda Desemba 9, 1961.

Chanzo: habarileo.co.tz