Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tamwa: Tusingashae wanafunzi wakimaliza darasa la saba hawajui kusoma, kuandika

88768 Tamwa+pic Tamwa: Tusingashae wanafunzi wakimaliza darasa la saba hawajui kusoma, kuandika

Tue, 17 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Joyce Shebe amesema hakuna haja ya kushangaa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu wakati takwimu zinaonyesha bado Tanzania inakabiliwa na tatizo la udumavu.

Udumavu ni ugonjwa unaotokana na kukosekana kwa lishe bora ambayo madhara yake makubwa ni kudumaa kwa akili na uwezo wa kufikiri.

Utafiti wa Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) kuhusu lishe za mwaka 2018 zinaonyesha Tanzania ina wastani wa asilimia 31.8 ya watoto waliodumaa.

Joyce amesema hayo leo Jumatatu Desemba 16, 2019 wakati akizungumza kwenye kongamano kuhusu Haki za Mtoto lililoandaliwa kwa pamoja baina ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Amesema ikiwa taifa halitachukua hatua madhubuti kupambana na udumavu litarajie kufikia maendeleo kiuchumi ikiwa watoto hao wataendelea kukosa lishe bora.

“Usishangae kuona mtoto hajui kusoma wala kuandika, unashangaaje wakati mtoto huyo hajapata lishe bora na ya uhakika wakati wa ukuaji wake wa awali?” amesema Joyce.

Mwenyekiti huyo wa Tamwa amesema lazima kila mmoja kwenye nafasi yake asimame na kuhakikisha jamii inajua namna ya kuwapatia watoto lishe bora.

Amewataka wanawake kuwanyonyesha watoto wao bila visingizio vyovyote kwa sababu ni ukweli usiopingika kuwa maziwa hayo husaidia kwenye ukuaji wa ubongo wa mtoto.

Joyce ametoa mfano kwa nchi ya China kwamba inajivunia uwingi wa watu wake kwa sababu, waliwekeza kwenye lishe na wanauwezo wa kufikiri.

“Uwingi wa watu wetu tunawezaje kujivunia ikiwa tutaandaa watoto wasio na lishe, wenye udumavu na ambao hawataweza kufikiri sawasawa?” amesema Shebe.

Ameshauri kuwapo kwa mkakati madhubuti utakaosaidia kila mtoto anayezaliwa anapata lishe bora.

Mtaalamu kutoka Idara ya Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka Shirika la kuhudunia watoto Dunia (Unicef), Tuzie Edwin amesema uwekezaji wa ukuaji wa mtoto hasa kwenye masuala ya lishe ni muhimu katika kujenga uchumi wa nchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz