Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Tamko la kumtaka Rais CWT kujiuzulu ni batili’

Cet Geita Pic Katibu wa CWT Mkoa wa Geita, Lucy Masegenya akizungumza na waandishi

Sat, 8 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Chama cha Walimu Mkoa wa Geita (CWT) kimesema waliotoa tamko la kumtaka Rais na Katibu wa Chama hicho kujiuzulu sio wasemaji wa chama kikidai kilichofanyika ni kinyume na taratibu, kanuni na katiba ya chama.

Julai 5, 2023 baadhi ya walimu mjini Geita walitoa tamko la kumtaka Rais wa CWT, Leah Ulaya na Katibu wake, Josephat Maganga kujiuzulu ndani ya siku 14 kwa kile walichodai viongozi hao wamekosa uadilifu katika utumishi pamoja na kuwatuhumu kuwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 8, 2023 Katibu wa chama hicho mkoani Geita, Lucy Masegenya amesema kilichofanywa na baadhi ya wanachama ni batili na kuwataka kufuata taratibu na miongozo iliyopo kwenye katiba ya CWT kutatua migogoro au changamoto zinapotokea.

Masegenya amesema tamko lililotolewa na wanachama hao ni batili na nikinyume na taratibu za chama kwa kuwa waliotoa tamko sio viongozi wala wasemaji wa chama na mazingira waliyotumia yalikua nje ya utaratibu.

“Mfumo wa chama cha walimu ni wa uwakilishi kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa kuna utaratibu wa vikao kwa ngazi zote na wasemaji wake ambao hutoa taarifa za chama, baada ya vikao halali kunamsemaji wa wilaya, mkoa na Taifa haya yaliyotokea ni batili,”amesema Masegenya

Akizungumzia fununu za baadhi ya wanachama kukihama chama, amesema katika ofisi yake hajapata taarifa za waliohama lakini imeendelea kuandikisha wanachama wapya ambao wameajiriwa hivi karibuni na kupangiwa vituo vya kazi kwenye mkoa huo.

Katibu wa CWT Wilaya ya Bukombe, Haruna Kambi amewataka wananchama kutojichukulia mamlaka na kutoa matamko yasiyo sahihi na badala yake wafuate taratibu kwa mujibu wa katiba inayotaka viitishwe vikao sahihi kuzungumzia malalamiko hayo.

Kwa mujibu wa katibu chama hicho hadi sasa kina wanachama 11,368 kati ya walimu 12,768 waliopo mkoani Geita.

Chanzo: Mwananchi