Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Talaka zashamiri Ruangwa, ndoa za ‘mashindano’

37950 Pic+talaka Talaka zashamiri Ruangwa, ndoa za ‘mashindano’

Wed, 23 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa. Kinamama katika kata ya Likunja wilayani Ruangwa wamelaumiwa kuwa ndio chanzo cha kuvunjika kwa ndoa kila kukicha katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo lililopo mkoani Lindi, kasi ya wanandoa kuachana ni kubwa, na hata ile ya kuoana nayo ni kubwa hasa msimu wa mavuno.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Likunja, Maria Lilai alisema ndoa zinavunjika kwa sababu ya mfumo wa mama kuwa na madaraka kwenye familia zaidi ya baba.

“Mfumo huu ambao unampa mama madaraka ya kuwa kichwa cha familia ndiyo unaofanya ndoa nyingi zinavunjika, kwa sababu wanaume wengi hawapendi kuwa chini ya mwanamke, hivyo migogoro mingi inaishia kwenye talaka,” alisema mwalimu huyo wakati wa mafunzo ya wanakamati za ulinzi za kata hiyo yaliyotolewa na Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Alisema matukio ya kutolewa talaka ni ya kila uchao, lakini zipo kesi ambazo wanandoa wanatengana ingawa wanaume hukataa kutoa talaka.

“Akikataa kutoa talaka inabidi (mwanamke) uinunue, wapo wanaume ambao hukataa kutoa talaka hadi uwape hela. Ukiwapa hela wanakupa talaka yako.”

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa kata hiyo, Sarah Pongolela alisema kwa mila za kabila la Wamwera mwanaume anapooa ni lazima amjengee mke wake nyumba.

“Mara nyingi migogoro hii inaanzia kwenye mgawanyo wa mali au pale ambapo kipato kinaongezeka,” alisema Sarah.

Alisema hakuna takwimu rasmi za matukio ya talaka kwa sababu mengi yanamalizikia katika ngazi ya familia.

“Matukio mengi yanamalizwa baada ya wanandoa kugawana mali, lakini kama kuna mgogoro zaidi ndipo unapofikishwa kwenye ofisi za kata au Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu) ama mahakamani,” alisema.

Akizungumzia matukio ya talaka, mwenyekiti wa chama cha kinamama katika kata hiyo, Shelly Nachinuku alisema yako mengi, lakini anadai chanzo ni wanaume.

“Kesi hizo zinaanzia kwa wanaume, mfano mwanamume akishaona amemzalisha mwanamke anamuacha au akiona kuna watoto wengi ndani ya nyumba anakuacha na anaenda kwa mwanamke mwingine,” alisema.

Alisema suala la talaka linachangiwa na wanaume kutokaa nyumbani na kutotimiza majukumu yao kwenye familia.

“Wanaume wanapoona msimu wa mavuno wanazikimbia familia zao na kudai wanakwenda kuangalia mazao kumbe wanayauza na kuanza kutumia fedha na wanawake wengine.”

Alisema hata shuleni imebainika wanafunzi wengi wanalelewa na mzazi mmoja au bibi baada ya wazazi wao kuachana.

Katekisti wa Kigango cha Kanisa Katoliki Likunja, Erick Akwilambo alisema kesi za wanandoa kuachana eneo hilo husababishwa na ‘mfumo jike’ ambapo wanawake wanakuwa na madaraka makubwa kwenye familia.

“Ndiyo maana hata hizi kesi za wanaume kupigwa ni nyingi huku wanaume hawana la kusema, hata mtoto akizaliwa anakuwa ni wa ukoo wa kwa mama,” alisema.

Kwa upande wake, ofisa Elimu wa kata hiyo, Mwajuma Ibadi alisema siyo talaka tu, bali hata ndoa zinafungwa kwa wingi kama ilivyo talaka.

Alisema wakazi wa eneo hilo wanafunga ndoa nyingi “utadhani ni za mashindano.”

“Kwa mfano, wanandoa wakiachana, basi kila mmoja atataka aoe au aolewe tena ili kumkomoa mwenza waliyeachana,” alisema Ibadi.

Alisema asilimia 70 ya wanafunzi wa shule za msingi wanalelewa na bibi au babu baada ya wazazi wao kutengana na kwamba, suala hilo ni miongoni mwa mambo yanayochangia ndoa za utotoni.



Chanzo: mwananchi.co.tz