Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yawezesha ujenzi wa nyumba mpya kwa mjane

884529a7a82e07bb5a986bdbfa6e2171 Takukuru yawezesha ujenzi wa nyumba mpya kwa mjane

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa imewezesha mama mjane, Usna Joseph kujengewa nyumba mpya baada ya kiwanja alichokuwa akimiliki yeye na mume wake kuuzwa katika mazingira ya kutatanisha.

Nyumba hiyo inayokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 40 imejengwa na mnunuzi wa kiwanja hicho (hakutajwa jina) katika eneo la Kihesa KKKT, mjini Iringa na ilikabidhiwa juzi kwa mjane huyo aliyekuwa ameambatana na baadhi ya watoto wake.

Akizungumza na wanahabari juzi, Kamanda wa Takukuru mkoa wa Iringa, Domina Mukama alisema kiwanja cha mjane huyo ambacho tayari kimeendelezwa na mnunuzi huyo, kipo katika eneo la Gangilonga linalokaliwa na viongozi na watu mbalimbali wenye uwezo.

“Baada ya Takukuru kuingilia kati mgogoro huo, tuliingia makubaliano yaliyowezesha mnunuzi wa kiwanja hicho kumjengea nyumba mpya mjane huyo, kazi ambayo tayari imekamilika,” alisema.

Akiishukuru Takukuru kwa kumsaidia kumjengea nyumba hiyo mjane huyo na kusema, “ nilifikisha taarifa ya kiwanja chetu kuvamiwa baada ya kuona kuna ujenzi unaendelea bila mimi mwenyewe kujua.

Baada ya Takukuru kuifanyia kazi taarifa tulikutanishwa na mnunuzi wa kiwanja hicho aliyeuziwa bila yeye kujua na kukubali kumfidia kwa kumjengea nyumba hiyo mpya.”

Kamanda huyo wa Takukuru aliwataka wananchi wengine wenye malalamiko yanayofanana na hayo wayafikishe katika ofisi zao ili yaweze kushughulikiwa kwa kuzingatia sheria.

Mukama alisema katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2020, walifanikiwa kuokoa zaidi ya Sh milioni 586.6 zilizokusanywa kutoka kwa wadaiwa sugu wa saccos, vyama vya ushirika, benki na wakopeshaji binafsi katika wilaya zote za mkoa wa Iringa.

Aidha katika kipindi hicho, Mukama alisema Takukuru imefanikiwa kuokoa vifaa ghafi vya umeme vya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) vyenye thamani ya Sh Bilioni 1.2 kutoka kwa wakandarasi mbalimbali waliokuwa wakitekeleza miradi ya umeme vijijini (REA)

Chanzo: habarileo.co.tz