TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma imebaini hasara ya zaidi ya Sh milioni 16 zilizolipwa kwa walimu wasiostahili malipo wakiwemo wastaafu, waliofariki dunia na waliofukuzwa kazi na watoro wa muda mrefu.
Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Mpwapwa, Julieth Mtuy alisema Takukuru imefanya uchambuzi wa mfumo kuondoa walimu wasiostahili kwenye malipo ya mshahara mwaka jana ambapo jumla Sh milioni 3.75 zilirejeshwa.
Aliainisha chanzo cha walimu waliostaafu kuendelea kulipwa mishahara ni pamoja taratibu ndefu za kuchukua hatua za kinidhamu, ucheleweshaji wa utoaji wa taarifa za walimu wanaopaswa kuondolewa kwenye mfumo wa mshahara na uzembe kwa watumishi wanaohusika na mfumo wa malipo ya mshahara.
Kuhusu rushwa ya ngono, alisema Takukuru Wilaya ya Mpwapwa imekuwa ikitoa elimu ambapo kuna klabu za wapinga rushwa ngazi ya shule za msingi na sekondari.