Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yaokoa mil. 134/- ada Mazinde Juu

TANGAMAZ.webp Takukuru yaokoa mil. 134/- ada Mazinde Juu

Sat, 30 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeokoa Sh. 134,500,000 zilizotarajiwa kukusanywa na Shule ya St Mary's Mazinde Juu, wilayani Lushoto kutoka kwa wazazi na walezi kwaajili ya malipo ya ziada ya ada kabla ya Juni mosi, siku ambayo wanafunzi wa kidato cha sita wanatarajia kuanza rasmi masomo baada ya kusimama kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona.

Akizungumza jana, Mkuu wa Takukuru, Mkoa wa Tanga, Dk. Sharifa Bungala, alisema taasisi hiyo ilipokea malalamiko kutoka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo kidato cha sita, kwamba wamepewa maagizo kupitia kundi la ‘WhatsApp’ la wazazi na walezi kuanza kulipa fedha za ziada kabla ya kuanza kuwarudisha watoto wao shuleni kuanza masomo.

Bungala alisema malalamiko hayo yalikuwa yakimtuhumu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo. "Wazazi na walezi walilalamikia mkuu wa shule hiyo kuwa amewaagiza waanze kulipa kiasi cha Sh. 750,000 kwa kila mwanafunzi kabla ya Juni mosi, inadaiwa kuwa fedha hizo zilikuwa ni kwaajili ya kuwalipa walimu na wafanyakazi ambao watakuwapo katika kipindi hiki wanafunzi wakiwa shuleni kujiandaa na mitihani ya kuhitimu kidato cha sita."

Alisema suala hilo la malipo ya ziada lilionekana kuwakera wazazi na walezi wenye wanafunzi. "Wazazi wengi hawakufurahishwa na kitendo hicho kwasababu wengi wao wanaeleza kuwa walikuwa wameshalipa ada inayotakiwa kabla ya kufungwa kwa shule baada ya kuibuka kwa janga la corona na kimsingi hawakutakiwa kudai malipo ya ziada."

Malalamiko mengine ya wazazi na walezi ni kuhusu malipo ambayo walishayalipa Sh. 100,000 kwa kila mwanafunzi ili wabakie shuleni hapo kwa ajili ya kujiandaa na mitihani wakati wa likizo.

Kufuatia malalamiko hayo, Takukuru ilifanya ufuatiliaji kwa kuwasiliana na uongozi wa shule hiyo na kuthibitisha kuwa tuhuma hizo ni za kweli na kwamba wazazi na walezi wa wanafunzi 178 kati ya 222 wa kidato cha sita walitakiwa kulipa kiasi hicho fedha Sh. 750,000 kabla ya kufunguliwa kwa shule.

“Wanafunzi 44 wanaosoma shuleni hapo malipo hayo hayakuwahusu kwa kuwa wana ufadhili wa shule na wafadhili mbalimbali," alisema Bungala.

Alisema Sh. 133,500,000 zilitarajiwa kukusanywa na shule hiyo kutokana na malipo hayo na tayari wazazi wa wanafunzi wanne walikuwa wameshalipa jumla ya Sh. 3,000,000.

“Tulipouhoji kwa lengo la kupata ufafanuzi wa tuhuma hizo, Mkuu wa shule hiyo alisema wazo la malipo hayo lilifanywa na wazazi na walezi wenyewe kupitia kundi lao la WhatsApp na kwamba alikubaliana nao baada ya kuona kuwa ni jambo jema, lakini alipoona mjadala huo umekuwa mkali aliwaeleza kuwa malipo hayo siyo ya lazima bali atakayependa alipe na ambaye hawezi asilipe."

Alisema baada ya kuchambua maelezo ya Mkuu wa shule hiyo na ushahidi uliopatikana Takukuru na uongozi wa shule, walikubaliana baadhi ya mambo ili kuondoa malalamiko hayo ikiwamo kuandikwa kwa waraka wa kufuta mjadala huo wa malipo ya ziada ikieleza hakuna malipo hayo pamoja na kurejeshwa kwa fedha kwa wazazi na walezi ambao walikuwa wameshalipa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live