Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yamkabidhi muuguzi 8,000,000/- alizotapeliwa 2016

6d1a6257f255a615952977a6ca67bdc0 Takukuru yamkabidhi muuguzi 8,000,000/- alizotapeliwa 2016

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)Mkoa wa Dodoma jana iliwakabidhi jumla ya Sh 19,450,000 wakazi watatu wa jijini hapa akiwemo muuguzi mstaafu aliyetapeliwa zaidi ya Sh 8,000,000 na taasisi mikopo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alisema wamefanikiwa kumrejeshea muuguzi mstaafu, Grace Kusevya (64) jumla ya Sh 8,690,000 zikiwa ni fedha alizokuwa anaidai JW Micro Credit tangu mwaka 2016.

Alisema ufuatiliaji wa Takukuru, ulionesha Kusevya aliipatia kampuni hiyo Sh milioni 20 kwa ahadi ya kulipwa fedha hizo na fidia. Lakini, si tu kwamba hakulipwa faida yoyote, bali pia hata fedha yenyewe alilipwa sehemu tu hadi walipoingilia kati na kulipwa kiasi kilichosalia.

Pia alisema Dismas Kweka, mfanyabiashara na mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma amerejeshewa Sh 9,700,000. Alisema fedha hizo zimerejeshwa na Richard Mwambaje.

Kibwengo alisema awali Kweka aliuziwa kiwanja kilichopo Mbwanga kinyume na utaratibu, kwani kiwanja hicho kilitolewa na mwananchi mmoja kama sadaka kwa Jumuia ya Uamsho wa Wakristo Tanzania (UWATA) na Mwambanje alikuwa Katibu wa UWATA na alipokea Sh milioni 19 baada ya kutengeneza mkataba wa kughushi.

Alisema Mwambanje anatakiwa kurejesha kiasi kilichobakia wakati uchunguzi unaendelea. Alisema kuwa awali alishatoa Sh milioni mbili. Alisema kuwa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kiwanja hicho kimerejeshwa kwa UWATA.

Pia Takukuru imemrejeshea mwananchi mmoja Sh 1,060,000 alizotapeliwa na Job Makasi (43) mkazi wa Ipagala, ambaye aliahidi kumuuzia kiwanja kwa Sh milioni 13 lakini alikata mawasiliano tangu Agosti mwaka huu, baada ya kupokea malipo ya awali hadi alipotiwa nguvuni.

Aidha, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji, taasisi hiyo imewarejeshea viwanja vya wananchi watano, ambao walidhulumiwa na wengine waliodai wangewapa maeneo, ambayo hata hivyo yalikuwa tayari yana wamiliki wengine.

Hali kadhalika, Takukuru imerejesha serikalini Sh milioni 45.7 ikiwa ni sehemu ya fedha zilizolipwa kinyume na utaratibu wakati wa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Kijiji cha Mlongia wilayani Chemba.

Kibwengo alisema ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ulionesha kwamba mkandarasi wa mradi huo wenye thamani ya Sh. 579,323,000 ni kampuni ya Leostart Engineering ya Jijini Dar es Salaam. Alisema CAG alibaini pia kuwa mradi huo ulianza mwaka 2013 na kukamilika 2014 na mkandarasi alilipwa fedha zaidi ya kazi zilizofanyika, hivyo alitakiwa kuzirejesha.

Pia alisema Takukuru imeweza kuokoa na itarejesha kwa Uhamiaji Saccos eneo lenye ukubwa wa ekari tano lililopo Ihumwa. Alisema ufuatiliaji wao umeonesha kuwa mwaka 2017 Ezekiel Mchemwa aliuza eneo hilo kwa Uhamiaji Saccos kwa Sh milioni 65 lakini baadae akauza kwa watu wengine.

Aliwataka wakazi wa Dodoma kuwa makini wanapotaka kununua ardhi.

Chanzo: habarileo.co.tz