Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, imeanza uchunguzi kwa baadhi ya miradi inayotekelezwa katika wilaya sita za mkoa huo.
Pia, Jeshi la Polisi hapa nalo limeshawahoji baadhi ya watu, wakiwemo watumishi kutoka halmashauri mbalimbali za mkoa huo, huku wengine wakihojiwa na mamlaka zao za kinidhamu.
Uchunguzi huo unafanyika kutokana na maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda aliyotoa katika ziara zake alizofanya kwenye wilaya sita za mkoa huo.
Makonda aliagiza Takukuru kuchunguza baadhi ya miradi, ikiwemo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Samia iliyopo wilayani Longido.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Juni 10, 2024, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema uchunguzi umeanza katika maeneo yote yalikotolewa maagizo.
"Sehemu zote za wilayani ambako mkuu (Makonda) aliagiza uchunguzi ufanyike tumeanza kufanya. Ila siwezi kusema tuko katika hatua gani,” amesema.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amesema wameshawahoji watumishi kadhaa (hakutaja idadi yao).
“Ni kweli watu kadhaa walikuwa wanahojiwa na Polisi. Wengine walikuwa wanahojiwa na mamlaka zao za kinidhamu katika halmashauri zao,” amesema Kamanda Masejo.
Akiwa wilayani Longido, Makonda aliagiza kuundwa timu ya kuchunguza miradi yote inayotekelezwa wilayani humo, ikiwamo wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Samia.
Serikali imeshatoa Sh3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo iliyotakiwa kukamilika Machi, 2024.
Hata hivyo, Masejo amesema majengo yote yamekamilisha isipokuwa bwalo la chakula ambalo linatajwa kugharimu Sh460 milioni.
Wilayani Karatu aliagiza kufanyika uchunguzi baada ya kubaini kuna watumishi waliotengeneza risiti bandia za kielektroniki (EFD) na kuzitumia kukusanya mapato kwa wafanyabiashara wa samaki aina ya kabayo katika eneo la Mang'ola.
Baada ya maelekezo hayo, Jeshi la Polisi lilimshikilia mhasibu mmoja wa halmashauri ya Karatu, huku likimsaka mwenzake anayedaiwa kushirikiana naye kukusanya mapato katika chanzo hicho cha halmashauri.
Kutokana na sababu hiyo, halmashauri hiyo imesema kutafanyika uchunguzi katika vyanzo vyake vyote vya mapato, ili kubaini kama kuna uchepushwaji wa makusanyo ya mapato hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Juma Hokororo amesema Mei 23, 2024, walibaini watumishi hao wawili wametengeneza mfumo mwingine unaotoa risiti bandia za EFD zinazoonyesha zimetolewa na halmashauri hiyo.
Alisema katika eneo hilo, gari moja hutozwa ushuru wa Sh1.5 milioni ila wao walikuwa wanatoza Sh1 milioni na kutoa risiti bandia na fedha hizo kutoingia kwenye mfumo wa halmashauri.
Katika Halmashauri ya Monduli, aliagiza uchunguzi ufanyike sambamba na kuwachukuliwa hatua watumishi wanane wanaodaiwa kula Sh52 milioni, huku Arumeru akiagiza kukamatwa kwa Ofisa Mtendaji kata ya Bwawani, Simon Kaaya anayetuhumiwa kuwa chanzo cha migogoro katika kata hiyo.
Wakati huohuo, Takukuru imeeleza kubaini watumishi wawili wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, wakidaiwa kuhusika na tuhuma za kughushi nyaraka, uchepushaji wa makusanyo ya Serikali na ubadhirifu wa fedha za umma, wakidaiwa kutengeneza namba bandia ya mlipakodi na kampuni hewa ya kulipia makusanyo hayo.
Uchunguzi huo umefanywa kutokana na tuhuma zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo kudai kulipa kodi ya huduma Sh24 milioni, lakini akapewa risiti ya Sh3.6 milioni.