Kisarawe. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani imemfikisha katika mahakama ya wilaya hiyo mwenyekiti wa shirika la Kingonet, Ramadhan Sung'he kwa makosa manane, akidaiwa kujipatia Sh10 milioni kwa kughushi nyaraka.
Akisoma mashtaka hayo leo Desemba 3, 2018 mbele ya hakimu mfawidhi wa wilaya hiyo, Devotha Kosoka, mwendesha mashitaka wa Takukuru, Naftali Mnzava amesema Sung'he alijipatia fedha hizo akidai ni kwa ajili ya kununua Katiba wakati alikuwa akizipata bure.
Amesema kosa la kwanza kwa ni kufuja na kuchepusha Sh3.4 milioni kwamba Novemba 19, 2012 akiwa mwajiriwa wa Kingonet, alitumia fedha hizo katika miradi mbalimbali ya mtandao huo.
Amebainisha kuwa kosa la pili ni kughushi Sh1.2milioni ambazo mtuhumiwa alidai kununua makala 240 za Katiba ya Tanzania kinyume na kifungu cha 333, 335(a) na 337 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 marekebisho ya mwaka 3002.
Amesema kosa la tatu ni mtuhumiwa huyo kughushi nyaraka na kujipatia Sh1.2 milioni akidai kununua nakala 240 za Katiba za Jamhuri ya Muungano.
Katika shtaka la nne, mtuhumiwa huyo amedaiwa kughushi nyaraka za Kingonet na kujipatia Sh1.25 milioni akidai kununua nakala 250 za Katiba za Jamhuri ya Muungano, sawa na shitaka la tano.
Mnzava amedai mahakamani hapo kuwa Juni 11, 2013 mtuhumiwa alighushi nyaraka akidai kupata baraka za bodi ya asasi hiyo, alijilipa Sh200,000 kwa ajili ya matumizi ya uhasibu.
Amesema kuwa mtuhumiwa aliendelea kughushi nyaraka ambapo katika shitaka la saba, alichota Sh750,000 akidai kununua nakala 150 za katiba sawa na shitaka la nane ambalo pia alichota Sh750,000 akidai kununua Katiba.
Sung'he alikana makosa yote hayo na kutimiza masharti ya dhamana ya Sh10 milioni, kesi hiyo kuahirishwa hadi Januari 2, 2019.