Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru kutoa elimu Geita madhara utoroshaji dhahabu

67933087f85f60cc890fe7bfc64a60e1.png Takukuru kutoa elimu Geita madhara utoroshaji dhahabu

Thu, 24 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) Mkoa wa Geita imesema wanayatumia maonesho ya madini yanayoendelea mkoani humu kwa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na wadau wengine wa madini kuhusu madhara ya kutorosha dhahabu ikiwemo kutaifishwa madini hayo.

Ofisa Mchunguzi Mwandamizi wa Takukuru Mkoa wa Geita, Alfred John alisema sekta ya madini ni muhimu katika kukuza uchumi na ndiyo maana serikali imeamua kuanzisha masoko ya madini ili kudhibiti vitendo vya utoroshaji na kwa kufanya hivyo serikali inapata mapato na wachimbaji nao wanapata faida kwa kuuza kwa bei halali.

“Masoko ya madini yanaleta usalama wa madini yao lakini pia wanauza kwa bei halali, kwa mfano juzi tu hapa kuna raia wa kigeni alilazimika kulipa faini ya Sh bilioni saba baada ya kukubali kosa la kutorosha madini, kwa hiyo kupitia maonesho haya pia tunatoa elimu kwa wananchi si tu kuhusu umuhimu wa kutumia masoko ya madini, lakini pia na mambo mengine ikiwemo rushwa wakati wa uchaguzi na rushwa ya ngono,”alisema.

Mambo mengine ambayo Takukuru Mkoa wa Geita inashughulika nayo ni kudhibiti vitendo vya dhuluma na rushwa wanavyofanyiwa wachimbaji wadogo na wa kati kuhusu masuala ya kupata leseni za uchimbaji, vitalu vya uchimbaji na ubia usio haki na mikataba isiyo na tija.

John alisema Takukuru pia inashughulika na vyama vya madini ambavyo viongozi wake ni wabadhirifu, wananunua vifaa bandia au vya gharama isiyokusudiwa, lakini pia kudhibiti raia wa kigeni wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini au biashara ya madini bila kuwa na kibali cha kuishi na kufanya kazi hapa nchini.

Alisema hivi karibuni baadhi ya raia wa kigeni kutoka China walilazimika kulipa faini ya Sh milioni 654 kwa kuingia nchini bila kibali na kufanya kazi za uchimbaji madini bila kufuata utaratibu.

John alisema raia wengi wa China wako mkoani Geita wakijishughulisha na biashara ya madini na baadhi yao hufanya hivyo bila kuwa na kibali hali inayowafanya wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Chanzo: habarileo.co.tz