Tabora. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Tabora imepokea taarifa 105 za malalamiko huku 53 zikiwa za rushwa.
Akizungumza leo Jumatano Aprili 15, 2020 mkuu wa Takukuru mkoani humo, Musa Chaulo amesema taarifa nyingine 52 zilihusu makosa mengine yasiyohusiana na rushwa.
Alieleza hayo wakati akitoa taarifa za utendaji wa taasisi hiyo kuanzia Januari hadi Machi 2020, kwamba taarifa zote zinaendelea kufanyiwa kazi.
Amebainisha kuwa wamekamilisha uchunguzi wa majalada 13, kufungua kesi mpya tano na wameshinda kesi tatu.
Amezitaja kesi walizoshinda kuwa ni ya mhudumu wa afya hospitali ya rufaa ya Mkoa aliyeomba rushwa kwa ndugu wa mgonjwa ili aongezewe damu.
Nyingine ni ya ofisa wa kampuni ya udalali aliyeomba rushwa ili wasiuze nyumba ya mteja aliyekuwa anadaiwa na benki na nyingine ni ya mtu mmoja aliyeomba rushwa kwa aliyekuwa akidaiwa kumuua mkewe ili asifikishwe mahakamani.
Pia Soma
- Mtunzi wa vitabu Ken Walibora afariki dunia
- Wagonjwa wapya sita wa corona wabainika Zanzibar, mmoja afariki dunia
- Bila barakoa hakuna kuingia KCMC