Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru Mpwapwa yaanzisha kliniki tembezi kusaidia wa pembezoni

7b723a611b55483dfd242afc0e796597.jpeg Takukuru Mpwapwa yaanzisha kliniki tembezi kusaidia wa pembezoni

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, imeanzisha kliniki tembezi ya Kata kwa Kata kwa lengo la kuwafikia wananchi ambao hawana uwezo wa kufika makao makuu wilayani.

Akizungumza katika Kata ya Mima Kijiji cha Mima, Mkuu wa Takukuru wilaya ya Mpwapwa, Julieth Mtuy alisema lengo la kuanzisha kliniki tembezi ni kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kufichua kero yake.

"Sisi kama Takukuru tumeamua kuanzisha mfumo wa kuwafikia wananchi huku waliko kwenye kata na vijiji na tukiwasikiliza kero zao na kuwapatia majibu hapo hapo, tumekuwa tukiongozana na wataalamu mbalimbali wa halmashauri ya wilaya,"alisema.

Alisema katika utaratibu huo wamebaini kuwapo kwa kero ya fedha zinazotolewa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf) katika kijiji cha Mima hazijawafikia wahitaji.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Takukuru alimuagiza Mratibu wa Tasaf wilaya na timu yake kufika haraka katika kijiji cha Mima ili wafanye uhakiki vizuri na kuwapatia taarifa ofisini.

Kwa upande wao, wananchi wameipongeza Takukuru kwa kuanzisha kliniki tembezi kwani itawasaidia kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uwezo wa kusafiri hadi wilayani kutoa malalamiko yao.

Chanzo: habarileo.co.tz