Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru Ilala yaokoa Sh3.24 bilioni za makusanyo

FEDHA Takukuru Ilala yaokoa Sh3.24 bilioni za makusanyo

Fri, 27 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Ilala kwa kushirikiana na Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam imeokoa takriban Sh3.24 bilioni ambazo ni makusanyo mbalimbali ambayo hayakuwasilishwa benki kwa muda mrefu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini hapa alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji ya robo mwaka Julai hadi Septemba, 2023 Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Sosthetenes Kibwengo amezitaka mamlaka zinanazosimamia mapato ya Serikali kufuata taratibu husika.

"Wito wetu kwa wote wanaokusanya na kusimamia mapato ya Serikali ni kuwa matumizi ya fedha mbichi yameharamishwa na jinai haifi, hivyo tuzingatie taratibu za makusanyo na matumizi ya fedha za umma," amesema Kibwengo.

Kibwengo amesema walifuatilia utekelezaji wa miradi 11 ya maendeleo yenye thamani ya Sh10.45 bilioni katika sekta za ujenzi, elimu na barabara, ili kubaini na kuzuia uchepuzi wa vifaa na ucheleweshaji wa mradi na kukuza ushirikishwaji wa jamii pamoja na upatikanaji wa thamani ya fedha.

Aidha walibaini kasoro mbalimbali zikiwemo kutozingatiwa kwa mikataba ya ujenzi na kughushiwa kwa taarifa za vipimo vya ubora wa vifaa vya ujenzi.

Kibwengo amesema kupitia chambuzi mbili za mifumo ya usimamizi wa ukusanyaji wa kodi ya zuio na usimamizi wa ukusanyaji mapato katika soko la Ilala walibaini kwamba si kiasi chote cha kodi iliyozuiwa kiliwasilishwa Mamlaka ya Mapato (TRA) na wakati mwingine kilichelewa kuwasilishwa.

"Katika uchambuzi wa mapato katika soko hilo tulibaini kupotea kwa mapato mengi kutokana na rekodi potofu ya idadi ya wafanyabiashara ambapo wakati mwingine uhalisia wa idadi ni mara mbili au hata zaidi ya ile inayosemwa ambayo hutumika kukadiria kodi na tozo mbalimbali," amesema.

Akieleza mikakati ya robo mwaka Oktoba hadi Disemba Kibwengo amesema Takukuru Ilala itaendelea kujikita katika uzuiaji rushwa kupitia ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuchochea mabadiliko ya kimtazamo kwa kundi la vijana kupitia bonanza la michezo ya soka na pete kwa wanafunzi na wanachama wa klabu za wapinga rushwa wa shule za sekondari jijini hapa.

"Tutashirikiana na wadau watoa huduma kutoa mrejesho kwa wananchi wa kata kumi ambao walitoa kero zao kupitia utekelezaji wa Programu ya Takukuru Rafiki," ameongeza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live