Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru Dodoma yaeleza ilichobaini ukaguzi robo ya mwaka 2019

65072 Pic+taku

Tue, 2 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma nchini Tanzania, imesema jumla ya miradi 34 iliyokaguliwa na taasisi hiyo kuanzia Aprili hadi Juni mwaka 2019 ilikidhi matumizi ya fedha zilizotengwa.

Akizungumza leo Jumatatu Julai Mosi, 2019 jijini Dodoma, wakati akitoa taarifa ya Taasisi hiyo kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka, Mkuu wa Takukuru Mkoa huo, Sosthenes Kibwengo amesema matumizi ya fedha ya miradi hiyo yalionekana kufanyika vizuri  hivyo thamani ya fedha kupatikana.

Hata hivyo, amesema wamebaini viashiria vya jinai katika miradi minne na hivyo wameanzisha uchunguzi kuhusiana na uhalali wa malipo ya Sh1.409 bilioni yaliyofanyika katika miradi hiyo.

Amesema miradi iliyokaguliwa ipo katika sekta ya ujenzi wa miundombinu, afya, elimu na kilimo.

Amesema katika kipindi hicho taasisi hiyo ilipokea jumla ya taarifa 135 za rushwa na makosa mengineyo ambapo tuhuma kuhusiana na sekta ya ardhi zilikuwa asilimia 36, serikali za mitaa asilimia 31, polisi asilimia nane, kilimo asilimia sita, mahakama na ujenzi kila moja ilikuwa na asilimia nne huku asilimia 11 zilizosalia zilihusu sekta ya maji, maliasili, afya, madini, ukusanyaji wa mapato na sekta binafsi.

Amesema katika taarifa hizo kulikuwa na nyingine siyo za rushwa na zingine zilikuwa zinahusiana na rushwa hivyo zile zilizokuwa siyo za rushwa zilihamishiwa kwenye mamlaka husika na uchunguzi wa majalada nane ulikamilika.

Pia Soma

“Tumefungua mashauri saba mahakamani yakihusisha madiwani wawili, mtumishi wa kurugenzi ya mazingira, wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata, makarani wa mahakama na watendaji wa kata na vijiji,” amesema Kibwengo

Amebainisha kuwa mashauri mawili yalitolewa hukumu ambapo Jamhuri imeshinda shauri moja na katika shauri lingine mtuhumiwa aliachiwa huru na mashauri mengine 30 yanaendelea mahakamani.

Chanzo: mwananchi.co.tz