Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taharuki wananchi kukuta kaburi kiwanja cha askari

Thu, 7 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TAHARUKI imeibuka kwa wananchi wa Kitwiru Manispaa ya Iringa, baada ya kukuta kaburi jipya kwenye kiwanja walichodai ni cha askari wa usalama barabarani na kulazimika kuweka ulinzi wakisubiri lifukuliwe.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12 jioni baada ya wananchi wa eneo hilo kubaini uwapo wa kaburi hilo katika makazi ya watu ambalo lilikuwa limefukiwa siku mbili zilizopita.

Wakizungumza na Nipashe, wakazi wa eneo hilo waliokuwa wakishuhudia ufukuaji wa kaburi hilo chini ya usimamizi wa polisi, walisema eneo hilo ni la makazi ya watu na wameshangazwa kuona kaburi bila kujua nani wamefanya mazishi hayo.

Mkazi wa eneo hilo John Sanga, alisema kiwanja kilichokutwa kaburi kiliuzwa kwa askari mmoja na sababu za watu kufanya tukio hilo hazijafahamika.

Rose Ng'umbi, mkazi wa Nyamhanga B, ambaye ndiye mmiliki wa awali wa kiwanja hicho, alisema waliuza kiwanja hicho na hakuna mgogoro wowote wa eneo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyamhanga, Nasson Lusasi, alisema wamelazimika kuita polisi baada ya wananchi zaidi ya 1,000 kukusanyika katika eneo hilo toka juzi jioni kutaka kufukua kaburi hilo.

Alisema polisi walilifukua kaburi hilo lililokuwa na urefu wa mita mbili na kukuta chupa na jiwe.

Alisema tukio hilo linawachanganya kwa kuwa siku za hivi karibuni kumekuwapo na matukio ya watu kuuawa, na polisi wamefanikiwa kudhibiti.

Askari anayemiliki kiwanja hicho, Fatma Mkwawa, alisema alipigiwa simu kuelezwa kuhusu kaburi hilo katika kiwanja chake na kueleza kuwa waliofanya hivyo walikuwa wakijaribu kumtisha.

Diwani wa Kata ya Kitwiru, Baraka Kimata, alisema sababu ya wananchi kuweka ulinzi katika kaburi hilo ni kutaka kujua kilichozikwa ndani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, alisema baada ya kufukua hawajakuta kitu na kuwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa polisi wanapokuwa na mashaka na jambo ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live