Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taharuki mgomo wa mabasi Mbeya, Tunduma

 Bbd CRg.jpeg Taharuki mgomo wa mabasi Mbeya, Tunduma

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabasi yanayotoa huduma kati ya Mbeya na Tunduma yamegoma na kusababisha taharuki kwa wasafiri, huku magari binafsi, bajaji na wengine wakijaribu kusimamisha hata malori.

Mgomo huo ambao unadaiwa ulianza tangu wiki iliyopita kwa kupandisha nauli kimyakimya leo Jumatatu Oktoba 16, 2023 umekuwa mkubwa zaidi na kusababisha kero kubwa kwa abiria.

Mmoja wa abiria aliyekuwa akisafiri katika kituo kidogo cha Chaula mjini Vwawa, Faines Julius amesema amefika kutuoni hapo tangu saa 1:40 asubuhi lakini ameshindwa kupata usafiri kutokana na kinachodaiwa kuwa kuna mgomo wa mabasi yanayofanya safari kati ya Tunduma na Mbeya.

"Kabla ya kuja hapa niliingia stendi kuu Vwawa lakini kule nikaambiwa hakuna magari yanayoingia hapo na hivyo kulazimika kuja hapa ambapo hata hivyo hakuna mabasi, watu wengine wamelazimika kupanda magari madogo ambayo yanatoza nauli ya Sh6,000 badala ya Sh3,500," amesema Faines.

Said Kandonga mkazi wa Vwawa amesema ameshindwa kwenda kumuona mgonjwa wake ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kutokana na kukosekana usafiri uliosababishwa na kupanda bei ya nauli.

"Nimeshindwa kuendelea na safari kufuatia ukosefu wa mabasi, lakini wenzangu wengi tayari wamesafiri kwa kutumia usafiri binafsi ambao walitutangazia nauli kuwa ni Sh6,000, kwa kuwa sina hiyo hela nimeahirisha," amesema Kandonga.

Ofisa wa Latra Mkoa wa Songwe, Joseph Bulongo amekiri kuwapo mgomo huo licha ya mamlaka hiyo kuwasihi wasigome badala yake wasubiri Oktoba 17 ambayo ni siku ya kutoa maoni yao mbele ya Mamlaka ya Usafirishaji Nchi Kavu (Latra) jijini Dar es Salaam lakini wao wameanza leo.

"Licha ya mgomo huo tunashukuru magari mengine yanayotokea Sumbawanga, Kamsamba na kwingineko yanayokwenda Mbeya yanasaidia kupunguza tatizo," amesema Bulongo.

Ameongeza kuwa inaonesha chanzo cha mgogoro ni huko Mbeya ambako nako Serikali inashughulikia tatizo hilo.

Kwa upande wao wamiliki wa mabasi hayo walipotafutwa na Mwananchi hawakupatikana kwa kuwa inadaiwa wapo kwenye na kikao cha ndani na Mkuu wa Wilaya Mbeya pamoja na maofisa wa Latra kutafuta suluhu ya mgomo huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live