Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tahadhari ya upungufu wa maji yatolewa, imo Dar na mikoa mingine mitano

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bagamoyo. Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu imetahadharisha kwamba endapo hatua madhubuti za usimamizi wa rasilimali za maji hazitachukuliwa upo uwezekano wa kuongezeka kwa uhaba mkubwa wa maji katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Bodi ya Bonde la Maji la Wami Ruvu iliyoanzishwa mwaka 2002, inatekeleza majukumu yake katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Tanga, Dodoma na Manyara.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Hamza Sadiki amesema kwa  kawaida mahitaji ya maji kwa mtu mmoja kwa mwaka inatakiwa isishuke mita za ujazo 1,700  ila kwa sasa kutokana na changamoto zilizopo kuna tishio la kushuka kwa makadirio hayo na kuwa 1,500 ifikapo 2025 kwa mtu mmoja.

Sadiki amesema hayo leo Jumatatu Machi 25, 2019 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati akifungua warsha ya kuwajengea na kuwaongezea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya usimamizi rasilimali za maji nchini.

Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa mwaka 2014 maji yaliyokuwepo ni lita za ujazo 1,950 kwa mtu mmoja lakini kiwango hicho kimeshuka kwa kasi.

Amesema zipo dalili zinazoonyesha upungufu utakuwa mkubwa kwa sababu mahitaji yanaongezeka sambamba na uharibifu wa vyanzo pia kwenye maeneo kadhaa ya bonde hilo.

"Sisi Bonde la Wami Ruvu tuna changamoto za usimamizi rasilimali za maji mfano uhaba wa maji, uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji, ongezeko la matumizi ya maji, mipango isiyo ya pamoja ya maendeleo na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa hiyo hatua madhubuti za usimamizi na uendelezaji rasilimali za maji ni muhimu zichukuliwe kwa sasa zaidi," amesema.

Awali, mshauri wa masuala ya rasilimali za maji wa bonde hilo, Onesmo Zakaria amesema wanaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kutengeneza sera, sheria, miongozo, kanuni na taratibu mbalimbali za usimamizi wa rasilimali za maji ili huduma hiyo imfikie kila mmoja.

Pia wameandaa mpango wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji rasilimali za maji wa miaka 25 na wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa na usimamizi wa rasilimali hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz