Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tafiti na mbinu zinaendelea kupambana na kiwavijeshi

B Swal C Tafiti na mbinu zinaendelea kupambana na kiwavijeshi

Thu, 8 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Morogoro kinaungana na taasisi nyingine nchini katika kufanya jitihada za kumdhibiti mdudu aina ya kiwavijeshi vamizi ambaye alionekana nchini kwa mara ya kwanza katika mkoa wa Rukwa, Aprili 2017.

Kiwavijeshi huyu (Spodoptera frugiperda) ni mdudu ambaye anashambulia aina zaidi ya 80 ya mazao hasa katika ukanda wa kitropiki. Miongoni mwa mazao hayo ni mahindi, mpunga, mtama, mboga, jamii ya mikunde na pamba.

Asili ya mdudu huyo ni Amerika Kusini na Amerika ya Kati ambako amekuwepo kwa siku nyingi. Barani Afrika alionekana kwa mara kwanza mwaka 2016 huko Afrika Magharibi katika nchi ya Senegal.

Baada ya hapo akaonekana Afrika ya Kati na kisha akasambaa katika nchi nyingine za Afrika. Kiongozi wa timu ya watafiti wanaofuatilia udhibiti wa viwavijeshi vamizi katika chuo cha SUA, Profesa Gration Rwegasira anasema baada ya utafiti uliotangulia kuonesha wadudu hao wamesambaa kiasi gani, hatua iliyofuata ilikuwa ni kutafiti mbinu za kuwadhibiti.

Anasema utafiti wa awali ulifadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Anasema juhudi za kitafiti zinazofanyika kwa ufadhili wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) zinalenga kuwadhibiti wadudu hao na zinahusisha mbinu mbalimbali ikiwemo udhibiti husishi, matumizi ya viuatilifu hai na viuatilifu vya viwandani.

Anasema watafiti wanaandaa pia mfumo wa mawasiliano ya kompyuta na simu za mkono kumwezesha mkulima kumtambua mdudu huyo na kupata ushauri wa kitaalamu juu ya mbinu ipi atumie ili kumdhibiti.

Mfumo huo utakaojulikana kama ‘Faw Diagnostics and Management Advisory Tool’ unalenga kumwezesha mkulima kufanya utambuzi wa viwavijeshi kwa usahihi kwa kuangalia aina ya mashambulizi kwenye mazao au kwa kumchunguza mdudu mwenyewe.

Hatua hiyo itamwongoza mkulima kufanya uamuzi wa jinsi ya kuwadhibiti viwavi hao kulingana na hatua ya ukuaji, yaani umri ambao kiwavijeshi amefikia. Inaelezwa kwamba kiwavijeshi vamizi ana hatua sita za ukuaji na kadri anavyokua huongeza uwezo wa ukinzani dhidi ya viuatilifu.

Kuanzia hatua ya nne mpaka ya sita kiwavi hauawi kirahisi na aina nyingi za viuatilifu. Hivyo mkulima anatakiwa kuwianisha hatua ya ukuaji wa kiwavijeshi na kiuatilifu kinachofaa kwa kumchunguza anavyofanana au madhara aliyokwisha sababisha kwenye mazao.

“Mfumo huu unaoandaliwa sasa utamwezesha mkulima kufanya utambuzi na maamuzi ya udhibiti kupitia simu ya mkononi. Juhudi hizi za watafiti zimelenga kurahisisha utambuzi wa kiwavijeshi vamizi ambaye bado hajafahamika vema kwa wakulima wengi.

“Mfumo utamsaidia mkulima kufanya tathmini ya madhara na kufanya uamuzi sahihi juu ya mbinu za kumdhibiti kiwavijeshi huyu na hivyo kuepusha matumizi hasi ya viuatilifu yasiyozingatia kanuni za afya kwa viumbe hai na usalama wa mazingira,” anasema.

Kwa maelezo ya Profesa Rwegasira, inatazamiwa kwamba utafiti na uandaaji wa mfumo wa mawasiliano wa kompyuta na simu za kiganjani utakuwa umekamilika na kufanyiwa majaribio mwanzoni mwa mwaka kesho na hatimaye kuwa tayari kutumika mwishoni mwaka huo.

Anasema kwa kuwa mfumo utalenga pia kutumia viuatilifu, utafiti unaoendelea unaangalia pia ni viuatilifu gani ambavyo tayari vipo madukani vinavyoweza kutumiwa kirahisi na wakulima na kati ya hivyo ni vipi vina uwezo wa kumdhibiti mdudu huyo.

“Tunafahamu kwamba serikali hivi karibuni imesajili viuatilifu vingi dhidi ya viwavijeshi ila huwa inachukua muda viuatilifu vipya kumfikia mkulima na wakulima kuvizoea na kuvikubali.

“Wazo letu likawa twende mbele na tutafiti vile ambavyo tayari vipo madukani ambavyo wakulima wanavitumia mara kwa mara, tujue kati ya hivyo ni vipi vinaweza kumdhibiti mdudu huyu.

“Hivyo tulifanya utafiti tunaokaribia kuukamilisha ambao umeonesha aina ya viuatilifu ambavyo vimeweza kufanya kazi vema. Kwa hiyo tumetenga viuatilifu katika makundi kulingana na hatua ya ukuaji wa viwavijeshi na madhara ambayo mkulima anayoyaona shambani kisha tuweze kumshauri kirahisi,”

anasema. Anasema mfumo huo unamshauri mkulima aweze kuchukua hatua kulingana na anachokiona shambani na aweze kutumia dawa mwafaka na siyo tu aende dukani na kutaka kupewa dawa ya wadudu.

Anasema tabia ya wakulima wanapokwenda dukani husema wapewe dawa ya kuua viwavijeshi bila kuzingatia ni dawa gani sahihi.

Kwa maelezo ya Profesa huyo, mara nyingi wakulima wamekuwa wakilalamika kwamba wanapiga dawa lakini wadudu hao hawafi lakini wakati mwingine hilo linatokana na kukosa usahihi wa dawa gani itumike kulingana na kile kima cha ukuaji wa mdudu alichofikia.

Anakiri pia kwamba wagani maofisa ugani wengi lakini sio wote wanaoelewa juu ya wadudu hao na jinsi ya kuwadhibiti.

Mbinu nyingine anayoieleza ni kutafuta njia mbadala ya kudhibiti viwavijeshi vamizi hao kwa kuwa na wadudu rafiki kwani kuna jamii ya fangasi ambayo huwaua viwavi hao vamizi.

Anafafanua kwamba watafiti walizunguka mikoa mitano ya Rukwa, Morogoro, Dodoma, Manyara na Kilimanjaro na kukusanya jamii mbalimbali za wadudu na fangasi rafiki na kwamba kwa sasa wamewaweka katika maabara ya kuwazalisha kwa wingi iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

“Tunachokifanya tunaangalia uwezo wao wa kuwadhibiti viwavijeshi vamizi hao. Tukiona wanafaa tutawatengeneza katika hali ambayo wataweza kuuzika na kusambazika kirahisi kwa wakulima,” anasema.

Mwaka jana mkulima wa Kijiji cha Matala Kata ya Mwika Kusini, wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, Twaha Massawe ambaye ni mfano wa wakulima wengi nchini walioathirika na viwavijeshi vamizi alikiri kuwa wadudu hao ni tishio kubwa kwa wakulima.

Anasema kutokana na tishio la wadudu hao ilimlazimu kupiga dawa kila wiki mara moja mpaka mahindi yake yatakapochanua. Anasema katika ekari zake 2.5, mwaka jana alipata gunia 30 lakini kama isingekuwa viwavijeshi vamizi hao angepata gunia 40. Massawe ni mmoja wa wakulima wengi nchini ambao wamekumbwa na viwavijeshi.

Chanzo: habarileo.co.tz