Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tabibu adaiwa kujiua aacha ujumbe akiwaomba radhi wazazi wake

TabibuuA0002 Tabibu adaiwa kujiua aacha ujumbe akiwaomba radhi wazazi wake

Fri, 5 Apr 2024 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ofisa tabibu katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Geita, Fimbo Ncheye anadaiwa kujiua akiwa kwenye chumba alichokuwa amelala, huku akiacha ujumbe wa kuwaomba radhi wazazi wake kwa hatua alizochukua na kutaka mtu yeyote asilaumiwe juu ya kifo hicho.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Thomas Mafuru amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema ofisa tabibu huyo alikuwa akijitolea kwenye kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD) na hakuwa mgonjwa na hakuwahi kueleza iwapo ana tatizo lolote.

"Imetokea ghafla, tumepigiwa simu na kuambiwa mwenzetu amefariki kwenye chumba na hii ni kesi ya polisi, naomba nisieleze sababu za kifo. Hadi anaondoka kazini jana, alikuwa vizuri, hakuwa na shida yoyote. Ametibu wagonjwa bila shida, yaani hii imetokea tu ghafla," amesema.

Dk Mafuru amesema hadi sasa hawajafanya uchunguzi kujua chanzo cha kifo na kwamba wanasubiri taratibu za kipolisi pamoja na familia, ili mwili wake ufanyiwe uchunguzi.

Akizungumzia tukio hilo, mmiliki wa nyumba aliyofia ofisa tabibu huyo, Proses Mwiseo amesema saa tano usiku aligongewa na wapangaji wakidai wanasikia kelele za fujo kama mtu anaugulia na kuomba msaada, lakini walipofika walikuta kelele zimetulia na walipogonga hakufungua mlango.

Marco Madoshi, balozi wa shina namba tatu katika Mtaa wa Lwenge, amesema baada ya kutoa taarifa polisi walifika na kuvunja mlango na kumkuta kijana huyo yuko kwenye uvungu wa kitanda na ndani ya chumba kulikuwa na dawa zilizopondwa pamoja na dawa ya hospitali pamoja na sindano ambayo haijatumika.

Madoshi amesema hakuna anayejua sababu zilizochangia achukue uamuzi huo na kuwashauri vijana wakiwa na changamoto kuomba ushauri au kusema badala ya kuamua kujiua na kuacha familia ikiwa na majonzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro alipotafutwa na Mwananchi Digital amesema yupo kwenye ofisi nyingine na kuomba kupewa muda, ili afuatilie tukio hilo.

Chanzo: mwananchi.co.tz