Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taasisi za watu wenye ulemavu Tanzania zapewa ruzuku za mamilioni

Mon, 9 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Taasisi ya kimataifa ya Abilis Foundation iliyopo mkoani Arusha nchini Tanzania  imetoa ruzuku kwa vikundi 23 vya watu wenye walemavu ili kuweza kujikimu na kuacha kuwa wategemezi katika jamii.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 09,2019 msimamizi wa taasisi wa Abilis nchini Tanzania, Rafiki Msafiri  ambaye  ana ulemavu wa  kutokusikia amesema taasisi yao inajenga mwamko wa walemavu ili waweze kujisimamia wenyewe katika kupata mahitaji yao na kujitegemea kiuchumi.

Msafiri amesema taasisi hiyo, inatoa ruzuku kwa vikundi kuanzia watu watano  na inafadhiliwa na wahisani kutoka nchini Finland ikiwa chini ya wizara ya mambo ya nje.

"Tunatoa ruzuku kwa kikundi kwa mara ya kwanza kati ya Sh2 milioni hadi Sh6 milioni  na awamu ya pili kati ya Sh6 milioni hadi zaidi ya  Sh15 milioni na inaendelea kutokana na kutimiza masharti," amesema

Amesema kuna vikundi ambavyo vinapewa ruzuku maalum hadi Sh25 milioni ili kuweza kujikwamua katika umasikini kutokana na kuwa na miradi endelevu.

"Kuna taratibu zipo hadi kufikia sifa za kupata ruzuku hivyo tunatoa vito kwa wenye ulemavu kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili kuweza kunufaika na ruzuku hizi," alisema

Pia Soma

Advertisement
Rafiki alisema tangu kuanza kutoa ruzuku, taasisi yao imewafikia asilimia 85 ya watu wenye ulemavu ambao wanahitaji kujikwamua katika umasikini na kuacha kuwa tegemezi.

Hata hivyo, amesema changamoto ambayo wanakumbana nayo kwa sasa ni namna ya kuwafikia walengwa wote kwani baadhi hawana usafiri kufika kupata ruzuku na baadhi ya walemavu wana elimu ndogo ya utekelezaji wa miradi.

Baadhi ya watu wenye ulemavu, wakizungumza na mwananchi nje ya ofisi ya taasisi, huyo walieleza imekuwa ni mkombozi mkubwa kwao kwani sasa wanapewa ruzuku kupitia vikundi vyao na hivyo kuanzisha miradi.

Jeremiah Mollel amesema ingawa kikundi chao bado hakijakamilisha taratibu za kupata ruzuku lakini baadhi yao wamenufaika sana na taasisi hiyo ya kimataifa.

Taasisi hiyo licha ya kuwa na ofisi nchini Tanzania ina ofisi katika nchi ya Uganda, Ethiopia, Nepal, Vietnam na nchi nyingine kadhaa duniani.

Chanzo: mwananchi.co.tz